Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuchukue hatua kuepusha ndoa milioni 10 za utotoni kabla ya muongo kuisha- UNICEF

Mariama (kushoto) mwenye umri wa miaka 17 na Zeinabou mwenye umri wa miaka18 kutoka Niger wanasema walichukua hatua kuepusha ndoa ya mapema ya rafiki yao mwenye umri wa miaka 16.
© UNICEF/Juan Haro
Mariama (kushoto) mwenye umri wa miaka 17 na Zeinabou mwenye umri wa miaka18 kutoka Niger wanasema walichukua hatua kuepusha ndoa ya mapema ya rafiki yao mwenye umri wa miaka 16.

Tuchukue hatua kuepusha ndoa milioni 10 za utotoni kabla ya muongo kuisha- UNICEF

Haki za binadamu

Ripoti ya tathimini mpya iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF imeonya kwamba huenda kukawa na ndoa zingine za utotoni milioni 10 kabla ya kumalizika kwa muongo huu na hivyo kutishia miaka ya hatua zilizopigwa katika kupunguza ndoa hizo.

Katika kambi ya wakimbizi ya Hakimpara nchini Bangladesh tunakutana na binti Sonjida mwenye umri wa miaka 15 ambaye amelazimika kuolewa akiwa na umri huo mdogo.  Akiwa na mumewe mtu mzee anasema “ mwezi mmoja tu baada ya kuwasili hapa tulioana”. 

 

Wazazi wake hawakuwa na pesa hata ya kutoa mahari kulingana na mila na desturi zao kwa sababu ya changamoto za kiuchumi zilizochangiwa na janga la corona au COVID-19 

Sonjida anasema, “hatukuwa na fedha za kutosha na kwa kawaida wazazi wa msichana ndio hutoa mahari kwa familia ya muoaji, hivyo nisingeolewa naye nani mwingine angenioa?” 

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa jina “COVID-19: tishio kwa hatua zilizopigwa dhidi ya ndoa za utotoni” , kufungwa kwa shule, changamoto za kiuchumi, kuingiliwa kwa huduma , mimba na vifo vya wazazi kutokana na janga hili vinawaweka wasichana walio katika mazingira magumu katika hatari ya ndoa za utotoni. 

Ndoa za mapema ni moja ya sababu kuu za umaskini katika jami mbalimbali kote duniani. HalimŽ kutoka Chad aliozwa akiwa na umri wa miaka 14 na hakuwahi kwenda shule kabisa, tofauti na kaka zake ambao walipelekwa shuleni.
UNICEF/UN014189/Sang Mooh
Ndoa za mapema ni moja ya sababu kuu za umaskini katika jami mbalimbali kote duniani. HalimŽ kutoka Chad aliozwa akiwa na umri wa miaka 14 na hakuwahi kwenda shule kabisa, tofauti na kaka zake ambao walipelekwa shuleni.

Ripoti imeongeza kuwa hata kabla ya COVID-19 wasicha milioni 100 walikuwa katika hatari ya ndoa za utotoni kwenye muongo ujao  licha ya ndoa hizo kupungua kwa kiasi kikubwa katika baadhi ya nchi kwa  miaka ya hivi karibuni, kwa asilimia 15  kutoka msichana 1 kati ya 4 hadi msichana 1 kati ya 5 idadi ambayo ni sawa na ndoa milioni 25 zilizoepushwa, lakini sasa mafanikio hayo yako hatarini.  

 

Ripoti inasema wasichana wengi ambao wanaoolewa utotoni wanakabiliwa na changamoto lukuki za muda mfupi na za muda mrefu na wengi hukumbana na ukatili na pia kukatiza masomo hali ambayo ilimkuba Solange msichana mwenye umri wa miaka 17 kutoka Bertoua nchini Cameroon alipata ujauzito, akalazimika kuolewa na kukatisha masomo anasema “Sikutaka kuolewa , nilitaka kwanza kumaliza shule na sikuweza, sasa ninachotaka ni mwanangu Anne Martha akue na aende shule ili apate elimu nzuri.” 

 

Kwa mujibu wa ripoti janga la COVID-19 limezidisha adha ya ndoa hizo na duniani kote inakadiriwa kwamba wanawake na wasicha milioni 650 walio hai leo hii wamepitia ndoa za utotoni na nusu ya ndoa hizo zikitokea Bangladesh, Brazil, Ethiopia, India na Nigeria. 

 

Hivyo UNICEF inataka hatua madhubuti zichukuliwe sasa kabla hali haijawa mbaya zaidi.