Cameroon - Siku nzima na mchuuzi Christine Banlog

9 Machi 2021

Christine Banlog amekuwa mchuuzi kwa miaka 22 sasa. Yeye ni mjane mwenye umri wa miaka 64, na sasa analea wajukuu wake watatu huko Nyalla, kitongoji cha mji wa Douala nchini Cameroon.

Mwaka 2011, bintiye Christine alifariki dunia wakati akijifungua, na kumwachia watoto wake watatu wa kike, na mdogo kabisa wakati huo alikuwa na umri wa wiki moja. Hii leo wajukuu hao wana umri wa miaka 20, 15 na 10 na wajukuu hao ndio kichocheo cha maisha ya Christine.

Siku ya Christine inaanza saa 11 alfajiri, wakati muazini wa msikiti ulioko jirani anapokuwa ananadi swala.

Douala ni mji mkuu wa kibiashara wa Cameroon na ni mashuhuri sana kwa masoko yake ya jumla na rejareja. Christine ni mwanachama wa chama cha wachuuzi wanawake, ASBY, ambao ni mtandao wa kitaifa wa wanawake wanaonunua bidhaa jumla na kuuza rejareja. Nchini humo wanawawake hao wanajulikana kama "Bayem-Sellam".

Christine Banlog, baada ya kununua viazi vya jumla sasa anaelekea kwenye soko la kununua mboga mboga.
UN Women/Ryan Brown
Christine Banlog, baada ya kununua viazi vya jumla sasa anaelekea kwenye soko la kununua mboga mboga.

Tangu mwaka 2014, shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women limekuwa linasaidia chama hicho kwa kukipatia msaada fedha na mafunoz mbalimbali kwa wanawake wajasiriamali.

Kila asubuhi, Christine anawahi katika masoko mbalimbali kusaka bidhaa, baadhi ya masoko hayo yanahusika na viazi pekee, na mengine ni maarufu kwa ndizi mzuzu au mboga za majani. Yeye hununua mazao hayo na kufungasha kwenye kiroba na kisha kupakia katika bodaboda na kuhakikisha anafikisha kwenye soko la Nyalla ifikapo saa moja asubuhi. Katika eneo hilo la Nyalla, Christine ana eneo lake kuuzia. Nyakati za mapema ni nzuri na zina faida kwa kuwa anauza kwa bei nzuri na soko hufungwa saa tisa alasiri.

Kwa Christine, saa 9 alasiri ni mapema mno kumaliza kazi; Ana jukumu la kulisha watu wanne na mjukuu wake mkubwa amesajili kufanya mtihani wa kujiunga na shule hivyo anawajibika kulipa fedha. "Natumia kipato changu kulipa ada ya shule, ingawa ni vigumu mno, fedha haitoshi," anasema Christine.

Soko linapofungwa, Christine anachukua bidhaa zake na kuzipeleka kwenye genge lake lililo karibu na nyumbani ili kumalizia bidhaa zilizobakia.

Christine akiwa mbele ya genge lake karibu na nyumbani kwake huko Nyalla, nchini Camroon ambako huuza bidhaa zinazokuwa zimebakia pindi soko linapofungwa saa 9 alasiri.
UN Women/Ryan Brown
Christine akiwa mbele ya genge lake karibu na nyumbani kwake huko Nyalla, nchini Camroon ambako huuza bidhaa zinazokuwa zimebakia pindi soko linapofungwa saa 9 alasiri.

Kila mwezi, kwa wastani Christine hupata dola 54. Alianza mradi wake na mtaji wa dola 90. Hata hivyo faida inatofautiana kulingana na msimu wa biashara. Wakati wa msimu wa viazi, anaweza kupata faida ya asilimia kati 40 hadi 50.

Tangu ajiunge katika chama cha wanawake wachuuzi mwaka 2017, ameshuhudia faida ikiongezeka. Chama hicho kinawapatiwa mafunzo ya stadi za maisha na jinsi ya kusimamia vizuri fedha zake.

"Ndio, mafunzo yamenisaidia kuboresha biashara yangu. Kwanza wamenifundisha jinsi ya kutunza mtaji, kupanga matumizi na kupiga mahesabu ya faida," anasema Christine.

Alipoulizwa kuhusu changamoto kubwa, Christine anasema ni barabara ya vumbi ya kuelekea nyumbani kwake. "Tatizo la kwanza ni barabara tunayotumia. Barabara ni mbaya, wakati wa msimu wa mvua, mashimo yanajaa maji. Kwa sababu ya barabara mbovu nilianguka kwenye pikipiki na kuvunja mguu wangu."

Christine Banlog akirejea nyumbani kwa bodaboda akiwa na bidhaa alizonunua.
UN Women/Ryan Brown
Christine Banlog akirejea nyumbani kwa bodaboda akiwa na bidhaa alizonunua.

Christine hana bima, kwa hiyo iwapo hatofanya kazi sokoni kwa siku moja, basi anapata hasara.

Tatizo lingine ni kupata mkopo. "Nataka kununua kasha la kuhifadhia bidhaa zangu. Linagharimu dola 541 ambalo limetengezwa hapa nchini.." anasema Christine akiongeza kuwa iwapo atapata mkopo basi anaweza kununua kasha hilo na kupunguza gharama ya kusafiri kila siku kwenda kununua bidhaa mpya.

Mwisho wa siku Christine hurejea nyumbani ili kupika mlo wa usiku. "Nyumba ya mwanamke mchuuzi wa sokoni haikosi chakula. Chochote kilichobakia sokoni kinarudishwa nyumbani na kupikwa mlo wa usiku."

Na leo amepika supu ya samaki wa kukaushwa kwa moshi na bamia za kukaushwa.

Bamia zilizokaushwa ambazo Christine atatumia kutengeneza supu ya mlo wa jioni.
UN Women/Ryan Brown
Bamia zilizokaushwa ambazo Christine atatumia kutengeneza supu ya mlo wa jioni.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter