Kutoka kijana hatarishi hadi mkombozi wa vijana wenzake

8 Machi 2021

Nchini Tanzania shirika lisilo la kiserikali la Restless Development limekuwa jawabu kwa vijana wa kike na wa kiume ambao awali walionekana kuwa hatarishi katika jamii zao.

Miongoni mwao ni Ramlat Omar ambaye leo katika siku ya wanawake duniani tunafuatana naye katika simulizi yake ya kutoka hatarishi hadi mkombozi kwenye jamii yake.

Ramlat mkazi wa Temeke jijini Dar es salaam nchini Tanzania amezungumza na Ahimidiwe Olotu wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC jijini humo akisema “mimi kama Ramlat Omar ni mnufaika wa Restless Development kupitia mradi wa Mabinti tushike hatamu.” 

Yeye alijiunga na shirika hili akiwa anajitolea kwenye mradi huo wa mabinti tushike hatamu akifanya jukumu la uelimishaji rika husuan kwa mabinti na vijana wa kiume walioko mtaani. “Nilikuwa nafika maeneo ambako vijana wapo mfano kwenye vikao vyao vya bodaboda na pia nilikuwa natembelea nyumba kwa nyumba na kutoa ushauri na pia kuwafundisha jinsi gani wajitambue kama vijana. Pamoja na hayo nilikuwa nawafundisha pia masuala ya ujasiriamali.”

Ametoka wapi?

Ramlat anasema kuwa “mimi mwenyewe nilikuwa tatizo kwenye mtaa wangu. Kwa hiyo baada ya kupata hii nafasi Restless Development nikaona kuwa mimi mwenyewe nilikuwa napotea na pia nilkuwa napoteza wenzangu. Nilikuwa naweza kuondoka nyumbani asubuhi, nisiage na hata nisirudi na hata niko na wenzangu na tunakuwa tunajadili mambo yasiyo mazuri, mambo ya hatari."

Anasema aliona kuwa shirika hilo linaweza kunifikisha popote endapo "mimi nitafuata kanuni. Kama nimejua kudai haki zangu na kutunza afya yangu, kwa nini nisiweze kujiendeleza kiuchumi.”

Restless Development ikamuokoa

Kupitia shirika hilo, Ramlat alipata mafunzo ya ujasiriamali na hata sasa siyo tu anafundisha wenzake mambo mbalimbali kama vile kutengeneza chaki na batiki, bali pia anatembelea maeneo mbalimbali kusaidia wajasiriamali kuwa thabiti zaidi. “Nafundisha wajasiriamali mfano kama naona anashindwa kufanya vizuri. Nafundisha pia namna ya kusajili vikoba. Mimi ni mwalimu wa wajasiriamali. 

Mafanikio

Kimaisha hivi sasa Ramlat anatarajia kumiliki nyumba yake kupitia fedha anazopata kwa kutoa mafunzo na hata ujasiriamali na pia kufundisha vijana jinsi ya kuamua kufanya kile anachokitaka.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter