Wanawake wamesalia nguzo kuu hata katikati ya janga la COVID-19

Mereng Alima Bessela, mwenye umri wa miaka 50, ni mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa na anatoka eneo la Ntui, kwenye mkoa wa Kati wa Cameroon. Yeye ni mkulima wa kakao, zao ambalo kwa kawaida huwa ni kilimo cha wanaume pekee. Pia anamiliki mgahawa na a
UN Women/Ryan Brown
Mereng Alima Bessela, mwenye umri wa miaka 50, ni mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa na anatoka eneo la Ntui, kwenye mkoa wa Kati wa Cameroon. Yeye ni mkulima wa kakao, zao ambalo kwa kawaida huwa ni kilimo cha wanaume pekee. Pia anamiliki mgahawa na anafuga samaki.

Wanawake wamesalia nguzo kuu hata katikati ya janga la COVID-19

Wanawake

Hii leo ikiwa ni siku ya wanawake duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la COVID-19 limefuta maendeleo ya miongo kuelekea usawa wa jinsia huku wanawake wakikumbwa zaidi na machungu, bado kundi hilo limesalia kuwa mstari wa mbele kwenye hatua dhidi ya janga la Corona.

Katika ujumbe wake wa siku ya leo, Guterres amefafanua jinsi janga hilo limefuta maendeleo hayo akisema, “kuanzia kufutika kwa ajira hadi mlipuko wa kazi ya malezi isiyo na ujira, kuanzia kuvurugwa kwa shule hadi ongezeko la janga la ukatili majumbani na unyanyasaji, maisha ya wanawake yamepinduka, haki zao zimemomonyoka.Akina mama, hususan wasio na wenza, wamekumbwa na kiwewe kikubwa na machungu. Madhara yake yatadumu hata baada ya janga.”

Wanawake wamekuwa nguzo licha ya changamoto wanazopitia

Hata hivyo amesema wanawake hao hao licha ya wanayopitia, nao pia wamekuwa mstari wa mbele kwenye hatua dhidi ya hili janga.

Wamekuwa wafanyakazi muhimu wakiendelea kutunza wagonjwa, wakishikilia pamoja  uchumi, jamii na familia.

“Wao ni miongoni mwa viongozi ambao wameweka viwango vya ugonjwa chini na nchi kuwa kwenye mwelekeo wa kujikwamua,” amesema Guterres

Amegusia ujumbe wa siku ya leo unaoangazia nguvu ya mabadiliko itokanayo na ushiriki sawa wa wanawake.

“Tunaona sisi wenyewe kwenye Umoja wa Mataifa, ambako ninajivunia kuwa tumefikia usawa wa kijinsia kwenye nafasi za juu za uongozi ikiwa ni mara ya kwanza kwenye historia,” amesema Katibu Mkuu

Mradi wa mafunzo ya kilimo cha kisasa cha nyanya unaofadhiliwa na UNDP umebadilisha maisha Mara, Tanzania
UNDP/Sawiche Wamunza
Mradi wa mafunzo ya kilimo cha kisasa cha nyanya unaofadhiliwa na UNDP umebadilisha maisha Mara, Tanzania

Ushahidi uko dhahiri.

Guterres amesema pindi wanawake wanapoongoza serikali, tunaona uwekezaji mkubwa katika hiadhi ya jamii na ukwamukwaji mkubwa dhidi ya umaskini.

“Pindi wanawake wanapokuwa kwenye bunge, nchi zinapitisha sera thabiti zaidi za tabianachi. Pindi wanawake wanapokuwa kwenye meza ya mazungumzo ya amani, makubaliano yanadumu zaidi,” amefafanua Katibu Mkuu

Na sasa wanawake wakiwa ni idadi sawa ya uongozi wa juu kwenye Umoja wa Mataifa, tunaona hatua thabiti zaidi za kusaka amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu.

Guterres amesema katika tamaduni zilizokithiri mfumo dume, usawa wa kijinsia unakuwa ni hoja ya madaraka na wanaume wanaonekana kuwa sehemu muhimu katika suluhu.

Tweet URL

Je tufanye nini sasa?

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametoa wito kwa nchi, kampuni na taasisi kupitisha hatua mahsusi za kusongesha ushiriki sawa wa wanawake na kufanikisha mabadiliko ya haraka.

“Tunapojikwamua kutoka kwenye janga, mifumo ya usaidizi inapaswa kulenga wanwake na wasichana, ikiwemo kupitia uwekezaji katika biashara zinazomilikiwa na wanawake na sekta ya malezi. Kujikwamua kutoka kwenye janga, ni fursa yetu ya kuachana na vizazi vya kuenguliwa na ukosefu wa usawa,” amesema Guterres akiongeza kuwa, iwe ni katika kuongoza nchi, biashara au harakati, wanawake wanaleta mchango ambao unalenga maendeleo kwa wote na kuchochea maendeleo ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.

Amesisitiza kuwa sasa ni wakati wa kujenga mustakabli wa usawa, akisema, “hii ni kazi ya kila mtu na kwa maslahi ya kila mtu.”