Skip to main content

Je wajua utipwatipwa hupunguza nguvu za uzazi?

viazi vya kukaanga au chips na jibini. Kwa mujibu wa utafiti wa WHO kuna vifi milioni 17 kila mwaka vinavyosababishwa na maradhi ya moyo
Public domain
viazi vya kukaanga au chips na jibini. Kwa mujibu wa utafiti wa WHO kuna vifi milioni 17 kila mwaka vinavyosababishwa na maradhi ya moyo

Je wajua utipwatipwa hupunguza nguvu za uzazi?

Afya

Hii Leo ikiwa ni siku ya kukabiliana na utipwatipwa au unene uliokithiri, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, linasema ingawa siku hii ni tukio la kila mwaka, laini madhara ya janga la Corona au COVID-19 kuanzia mwaka jana yamefanya tukio hili kuwa na maana zaidi kuliko wakati wowote ule.
 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao kuadhimisha siku hii akisema janga la COVID-19 limenyemelea zaidi watu wenye utipwatipwa ambao wako katika hatari kubwa ya kulazwa hospitalini, halikadhalika hatari ya kuugua zaidi na hata kufariki dunia.

“Janga la Corona nalo limefanya kuwa vigumu kukabilana na utipwatipwa kwa sababu ni vigumu kwa watu kufanya mazoezi kutokana na hatua za kuepusha michangamano, huku hali ngumu ya kiuchumi na kuvurugwa kwa hatua za kusambaza vyakula kumepunguza uwezo wa watu kupata vyakula salama na vyenye lishe,” amesema Dkt. Tedros huku akisema kitendo cha watu kutengwa huongeza pia msongo wa mawazo na utipwatipwa kwa kuwa watu wengine wanaondoa msongo kwa kula zaidi chakula.

Takwimu za utipwatipwa duniani

Duniani kote, utipwatipwa umeongezeka mara tatu tangu mwaka 1975. Hadi mwaka 2016, zaidi ya watu wazima milioni 650 walikuwa tipwatipwa, saw ana asilimia 13 ya watu wazima wote duniani. Kiwango cha watoto wenye utipwatipwa nacho kimeongezeka zaidi ya maradufu katika miongo miwili iliyopita.

Athari za utipwatipwa

Athari za kiafya ni pamoja na magonjwa kama vile kisukari, moyo, saratani, msongo wa mawazo, kukosa nguvu za uzazi, magonjwa ya viungo vya ndani ya mwili, matatizo wakati wa kujifungua na mtu kushindwa kulala vizuri usiku.

WHO inasema watoto tipwatipwa wako na nafasi kubwa zaidi ya kuwa na kiwewe, msongo wa mawazo, kukumbwa na ukatili shuleni. Utipwatipwa na magonjwa na ulemavu ambavyo husababisha huwa na gharama za kiuchumi na kiafya, hupoteza tija na pia hudumaza uchumi.

Watoto wakipata mlo wa mchana shuleni nchini Burundi.
WFP/Hugh Rutherford
Watoto wakipata mlo wa mchana shuleni nchini Burundi.

Hatua za kuchukua

Dkt. Tedros amesema Baraza la Afya la WHO liliweka malengo ya kutokomeza utipwatipwa miongoni mwa watoto, mabarubaru na watu wazima lakini gonjwa la Corona linarudisha nyuma maendeleo yaliyopatikana hivyo akapendekeza mambo matatu ya kubadili mwelekeo.

Mosi kukabili utipwatipwa kupitia mbinu za afya ya umma kwa kuimarisha hatua za kuzuia, kudhibiti na kusimamia kama vile lishe bora wakati wa ujauzito na kusimamia uzito wa mama wakati wa ujauzito.
Wahudumu wa afya pia watoe mwongozo mzuri wa unyonyeshaji watoto hasa kwa familia ambazo zinakabiliwa na msongo. “Jukumu hilo la kusimamia unyonyesha lisisalie kwa familia pekee bali pia kwa waajiri sambamba na kusimamia milo ya watoto wachanga ili isiwe na sukari. Kwa bahati mbaya vyakula vingi vya watoto wachanga ikiwemo maziwa, uji vina sukari nyingi.”

Pili ni matumizi ya mbinu a kifedha kwa kuhakikisha milo yenye afya haitozwi gharama kubwa. Kwa hiyo serikali iangazie kodi na ruzuku na kusimamia mbinu za uuzaji wa bidhaa hizo. “Ni vyema tuelimishe familia na watoto kuhusu viwango vya lishe kwenye vyakula wanavyonunua ili hata na watoto wenyewe waelewe na faida zake.”

Hatua ya tatu ametaja ni kutumia mbinu za kitabibu kwa kuwapatia watoto na watu wazima wenye utipwatipwa huduma bora za afya.

Dkt. Tedros amesema kwa sasa WHO inaandaa mwongozo unaoweza kwenda na mazingira ya nchi husika ukitoa mapendekezo ya jinsi ya kutunza watoto na barubaru wenye utipwatipwa na watoto walio hatarini kupata utipwatipwa.

Amesisitiza kuwa kama ilivyo COVID-19, utipwatipwa nao unaweza kutokomezwa kwa hatua za kimataifa.