Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yafanya juhudi za kuwaokoa wanaoikimbia CAR kuingia DRC.

Wanawake na watoto wakimbizi wa ndani kwenye mji wa Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
Yaye Nabo Sène/OCHA
Wanawake na watoto wakimbizi wa ndani kwenye mji wa Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

UNHCR yafanya juhudi za kuwaokoa wanaoikimbia CAR kuingia DRC.

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linafanya kazi ya kuwahamisha maelfu ya wakimbizi wa Afrika ya Kati wanaoishi katika makazi ya muda mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwenda kwenye maeneo salama ambapo wanaweza kupata msaada wa kibinadamu na ulinzi.

Mamlaka nchini DRC zinakadiria kuwa wakimbizi 92,000 wamewasili kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, baada ya ghasia zinazohusiana na uchaguzi kuzuka miezi miwili iliyopita.  

Katika kambi ya wakimbizi huko Zongo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakimbizi wako katika makazi ya muda, yasiyoridhisha, duni, yaliyojengwa kwa makuti, na nyuso zao ni dhahiri zinaonesha hawana uhakika na kesho yao. 

Hata hivyo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linafanya kila namna kuyaokoa maisha ya wakimbizi hao na usajili unaendelea ili kuwatambua wapya wanaowasili na pia wenye mahitaji maalum. Watoto, vijana wanawake kwa wanaume, wanasubiri kusajiliwa kwa njia ya kielektroniki. Ouaki Paul ni miongoni mwa wakimbizi kutoka Afrika ya kati, kupitia lugha ya Sango, anaeleza hali ilivyokuwa akisema, "tulipowasili, hali yetu ya maisha ilikuwa ngumu, kupata chakula ilikuwa ngumu, hatukuweza kurudi huko kwa sababu usiku na mchana kulikuwa na kelele za risasi. Haiwezekani kurudi huko kwa sababu ukirudi huko na mambo yakatokea tena na yakakukuta huko, utasema nini? Hatuwezi kurudi nyuma, tutadumu hapa, mpaka Mungu atakapogusa moyo wa mtu kutusaidia. " 

Takribani wakimbizi 40,000 wamesajiliwa. Wana ufikiaji mdogo au hawana kabisa  maji ya kunywa, kujisafi, na chakula katika maeneo haya magumu kuyafikia karibu na mpaka. Wengine wamekaribishwa katika familia zinazowakaribisha, na ripoti zinaonyesha kwamba hadi familia tatu za wakimbizi zinaishi katika nyumba moja ndogo. 

Tiaani Kawa, ni Afisa habari wa UNHCR katika eneo hilo anasema, "tulifikiri kwamba kwanza tutakachofanya, tutatoa usaidizi haraka. Kwa mfano, kwa vitu visivyo vya chakula, kuwapa watu blanketi za kujifunika usiku dhidi ya baridi. 

Karibu theluthi moja ya watu milioni 4.7 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamelazimika kukimbia baada ya miaka ya mzozo unaojirudia.