Ulinzi wa amani ulienda sambamba na mafunzo ya mapishi kwa wanawake Darfur- Sajini-Taji Felista

4 Machi 2021

Tukiwa tunaendelea kumulika ripoti mbalimbali kuhusu wanawake kuelekea siku ya wanawake duniani wiki ijayo, tunarejea tena huko Darfur nchini Sudan kwa mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania Sajini-Taji Felista Temba.

 

Mlinda amani huyu mwanamke pamoja na kuwa ni mlinzi wa amani na mtaalamu wa afya kitaalamu ametumia pia fursa ya uwepo wake huko kupatia wanawake stadi za ujasiriamali ili hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi katikati ya mazingira ya mzozo.

Sajini Taji Felista anasema pamoja na jukumu kuu la ulinzi wa amani, hutoa huduma za matibabu kwa wananchi wa Menawash na magonjwa sumbufu ni Malaria, kuhara na vichomi na ndipo wakagundua ndipo wakagundua kuwa wananchi hawaelewi jinsi magonjwa hayo yanavyoambukiza hivyo waliwaelewesha lakini akatoa wito, akisema, “Umoja wa mataifa kupitia shirika lake la afya, WHO, kuelekeza nguvu zaidi kwa wananchi wa jimbo la Darfur ili waweze kujitambua na kujipatia wataalamu wake wenyewe wa afya katika magonjwa yanayowasumbua.”

Sajini Taji huyu akaenda mbali kuelezea sababu za wao kuwapatia wanawake wa Menawash Darfur stadi za ujasiriamali akisema kuwa, “Kulingana na uzoefu tuliokuwa nao na hawa wakimbizi wa ndani, tumeweza kubaini mapungufu waliyo nayo sisi wanawake walinzi wa amani. Tukaja na wazo kwamba tuwasaidie,tuwaelimishe ili waweze kuinua kipato chao. Kwa hiyo  tuliwezeshwa kufundisha darasa ambamo walijifunza masomo ya ujasiriamali; utayarishaji wa vitafunwa mbalimbali ambavyo vina ghrama nafuu kulingana na mahitaji yanayopatikana kwenye mazingira yao.”

Ametaja vitafunwa hivoy kuwa ni “maandazi, chapati, sambusa, kalimati pamoja na karanga za mayai. Baada ya kuwafundisha, wanaendelea kupika, kutumia na kuuza na kipato chao kinaendelea kupanda siku hadi siku.”

TANZBATT_13 ambacho ni kikosi cha mwisho cha Tanzania kwenye ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano  wa Afrika, UNAMID jimboni Darfur, tayari kinaondoka jimboni humo baada ya kumalizika kwa jukumu la UNAMID tarehe 31 Desemba mwaka jana wa 2020 kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter