Watoto waliotekwa na kuachiliwa Nigeria wanahitaji msaada wa hali na mali:UN

3 Machi 2021

Wataalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wamesema nchini Nigeria kumefanyika hatua kidogo sana za kuwasaidia vijana barubaru walioathirika na mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya shule na utekaji wa watoto.

Katika tahadhari waliyoitoa kandoni kwa kikao cha 46 cha Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva Uswis wataalam hao zaidi ya 12 wamesema “Bila msaada , waathirika ambao wameachiliwa wako katika hatari kubwa ya kudhulumiwa, usafirishaji haramu, ukatili wa kingono na mwingine wa kijinsia na mifumo mingine ya ukatili na machafuko.”

Hakuna tarifa zozote za uchunguzi wa uhalifu huo

Wataalam hao wamekosoa kukoseka kwa uchunguzi hadi sasa dhidi ya shambulio kwenye shule ya bweni iliyoko Kankara, Katika jimbo la Katsina ambako karibu wavulana 350 walitekwa na kuachiliwa baada ya siku kadhaa mwezi Desemba mwaka jana pamoja na kutochukuliwa hatua za kuzuia kurudia tena kwa kitendo kama hicho.

Wameongeza kuwa kumekosekana kabisa uwazi kuhusu mchakato wa kufanya uchunguzi dhidi ya uhalifu huo ikiwa sasa ni takriban miezi mitatu baadaye.

Mbali ya hayo hakuna huduma maalum ywa msaada wa kisaikolojia kwa waathirika hao tangu walipoachiliwa,wamesema wataalam hao na kuitaka mamlaka nchini Nigeria kuchukua hatua za muda mrefu ambazo zitarejesha ustawi wa watoto hao kimiwli na kiakili na kuwasaidia kukabiliana na unyanyapaa ambao mara nyingi unahusishwa na vitendo vya kutekwa.

Wataalam hao huru wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu wameelezea pia hofu yao kuhusu wasichana 279 ambao waliachiliwa Jumanne wiki hii baada ya kutekwa wiki iliyopita katika jimbo la Kaskazini Magharibi la Zamfara.

Wamesema vitendo hivi kwa kawaida vinatekelezwa na makundi ya watu wenye silaha na wahalifu ambao wanatarajia kupata fecha za harakahara kwa kuzilazimisha familia za waliowateka  na mamlaka kulipa kikombozi ili kuwaachilia mateka kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Na mara nyingi wanalenga taasisi ambazo hazidhibitiwi na serikali , zipo mbali na haswa maeneo ya vijijini.

Wengi wamepoteza masomo

Wataalam hao wamesema kwa sababu ya mashambulizi “Watoto wengi hawajarejea shuleni ba baadhi ya shule zimeshafungwa kabisa kwenye maeneo ya mpakani kwa sababu ya hofu ya kutokea tena vitendo vya utekaji. Hii inamaanisha mwisho wa masomo kwa watoto hawa.”

Tarehe 17 Februari mwaka huu watoto wengine 27 wanafunzi, waalimu watatu na watu wengine 12 walitekwa wakiwa chuoni kwenye jimbo la Niger na kuachiliwa siku 10 baadaye.

“Tunatiwa hofu na tarifa kwamba idadi siyojulikana ya wanawake na wasichana wametekwa katika miaka ya karibuni na huko wanakabiliwa na ukatili, kazi za shuruti, utumwa wa ngono kupitia ndoa za lazima, mimba za lazima na zisizotarajiwa,” wamesema wataalam hao.

Wataalam hao wamependekeza kuwe na programu maalum za kuwasaidia watoto hao, kuwapa msaada wa kisaikolojia na kuwawezeha kurejea na kujiunga tena na jamii hususan wanawake na wasichana.

“Programu hizo zijumuishe msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha, ikiwemo kwa familia za watoto hao.”

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter