Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipuuze uwezo wa masikio kusikia, ni lulu - Dkt. Tedros

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linataka serikali ziwekeze katika huduma za kuepusha watu kupoteza uwezo wa masikio yao kusikia.
The London School of Hygiene & Tropical Medicine (LSHTM)/A. Smith
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linataka serikali ziwekeze katika huduma za kuepusha watu kupoteza uwezo wa masikio yao kusikia.

Tusipuuze uwezo wa masikio kusikia, ni lulu - Dkt. Tedros

Masuala ya UM

Leo dunia inaadhimisha siku ya usikivu wa masikio katika kipindi ambacho tayari ripoti mpya ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO imetahadharisha kuwa kufikia mwaka 2050 takribani watu bilioni 2.5 ulimwenguni watakuwa wanaishi na kiwango fulani cha kupoteza uwezo wao wa kusikia ikiwa hatua hazitachukuliwa mapema.

Idadi hiyo ya watu iliyotajwa na ripoti ya WHO, ni sawa na mtu 1 kati ya watu 4 atakuwa anakabiliwa na tatizo la usikivu, na kwa msingi huo, takribani watu milioni 700, watahitaji kutumia vifaa vya kusikilizia au tiba ya masikio na huduma nyingine za kurekeisha masikio yao.  

Ripoti imefichua kuwa ukosefu wa taarifa sahihi na mitazamo ya unyanyapaa kwa magonjwa ya sikio na upotezaji wa usikivu mara nyingi huzuia watu kupata huduma dhidi ya hali hizi. Hata miongoni mwa watoa huduma za afya, mara nyingi kuna upungufu wa maarifa juu ya kuzuia, kutambua mapema na kushughulikia upotezaji wa usikiaji na magonjwa ya sikio, kuzuia uwezo wao wa kutoa huduma inayohitajika. 

Vilevile WHO kupitia ripoti hiyo, imeeleza kuwa katika nchi nyingi, huduma ya masikio na huduma ya tiba ya usikivu wa masikio bado haijajumuishwa katika mifumo ya kitaifa ya afya na kupata huduma ni changamoto kwa wale walio na magonjwa ya masikio na upotezaji wa usikivu wa masikio.  

Tweet URL

Pia ripoti imeliweka wazi pengo katika uwezo wa mifumo ya kiafya katika upande wa rasilimali watu ambapo inaonekana katika nchi zenye kipato cha chini, takribani asilimia 78 ya nchi hizo zina wataalamu wachache wa masikio, pua na koo, ENT, kiasi cha mtaalamu mmoja kwa idadi ya watu milioni moja na nchi asilimia 93 wana chini ya mtaalam mmoja wa sauti anayeshughulikia usikivu wa masikio kwa watu milioni moja na nchi asilimia 50 wana mwalimu mmoja au zaidi wa viziwi, kwa viziwi milioni moja. WHO inasema pengo hili linaweza kuzibwa kupitia ujumuishaji wa huduma ya masikio katika huduma ya msingi ya afya. 

Utafiti huo unaenda mbali zaidi na kueleza kuwa hata katika nchi zilizo na idadi kubwa ya wataalam wa afya ya masikio na usikivu wa masikio, kuna usambazaji usio sawia wa wataalam. Hii sio tu inaleta changamoto kwa watu wanaohitaji huduma, lakini pia inaweka mzigo zaidi kwa kada zinazotoa huduma hizi. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO amenukuliwa akisema, "uwezo wetu wa kusikia ni wa thamani. Upungufu wa kusikia usiotibiwa unaweza kuwa na athari mbaya kwa uwezo wa watu kuwasiliana, kusoma na kipato. Inaweza pia kuathiri afya ya akili ya watu na uwezo wao wa kudumisha uhusiano."