Uharibifu wa misitu unatishia uhai wa wanyamapori na binadamu- Guterres

Jamii la kabila la watu wa asili ambao wanaishi kwenye misitu iliyo ndani zaidi nchini Jamhuri ya ya Congo, DRC.
UNICEF/Vincent Tremeau
Jamii la kabila la watu wa asili ambao wanaishi kwenye misitu iliyo ndani zaidi nchini Jamhuri ya ya Congo, DRC.

Uharibifu wa misitu unatishia uhai wa wanyamapori na binadamu- Guterres

Masuala ya UM

Misitu ni uhai na sio tu kwa binadamu na mazingira bali pia kwa asilimia 80 ya viumbe vyote vya porini, hivyo kutumia vyema na kuilinda ni kwa maslahi ya watu wote, sayari dunia na maendeleo amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya wanyamapori duniani inayoadhimishwa leo.

Bwana. Guterres amesema misitu husaidia kudhibiti hali ya hewa na maisha ya mamia ya mamilioni ya watu. 

Asilimia 90 ya watu masikini zaidi ulimwenguni wanategemea kwa njia fulani rasilimali za misitu. 

Na hii ni dhahiri haswa kwa jamii za watu wa asili ambazo zinaishi ndani au karibu na misitu na kuongeza kwamba,“Asilimia 28 ya ardhi ya dunia inasimamiwa na jamii za watu wa asili, ikiwemo moja ya misitu isiyobadilika kabisa duniani. Inawapa riziki na utambulisho wa kitamaduni. Matumizi mabaya ya misitu uathiri jamii hizi na kuchangia upotevu wa bayoanuwai na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Kila mwaka, tunapoteza ekari milioni 4.7 za misitu ikiwa ni eneo kubwa kuliko nchi ya Denmark na kilimo kisichoendelevu ni chachu kubwa.” 

Katibu Mkuu ametaja sababu nyingine kuwa ni usafirishaji haramu wa mbao duniani ambao huchangia hadi asilimia 90 ya ukataji miti katika baadhi ya nchi na hamasisha makundi ya uhalifu mkubwa zaidi wa kupangwa duniani. Amesisitiza kwamba, “Biashara haramu ya aina mbalimbali za wanyama pori ni tishio lingine, ambalo linaongeza hatari za magonjwa yatokanayo na wanyama, kama Ebola na COVID-19. Kwa hivyo, katika siku hii ya wanyamapori duniani mwaka huu, ninahimiza serikali, wafanyabiashara na watu kila mahali kuongeza juhudi za kuhifadhi misitu na viumbe vya misituni, kuunga mkono na kusikiliza sauti za jamii za misituni.” 

Amesema kwa kufanya hivyo, kutachangia kufikia malengo ya maendeleo endelevu kwa watu, sayari na ustawi.