Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuachana na makaa ya mawe ni jawabu kwa tabianchi- Guterres

Katika viunga vya mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott, bustani ya mapangaboi ya kuzalisha umeme kwa njia ya upepo  yanaonekana kwa mbali na ni jawabu sahihi katika kuwa na nishati rejelezi
UNDP Mauritania/Freya Morales
Katika viunga vya mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott, bustani ya mapangaboi ya kuzalisha umeme kwa njia ya upepo yanaonekana kwa mbali na ni jawabu sahihi katika kuwa na nishati rejelezi

Kuachana na makaa ya mawe ni jawabu kwa tabianchi- Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amehutubia mkutaon wa kila mwaka kuhusu kuondokana na matumizi ya makaa ya mawe duniani akitaja mambo makuu matatu ya kuzingatia ili kutekeleza hatua hiyo.

Guterres akihutubia kwa mtandao mkutano huo ulioandaliwa na Uingereza na Canada amesema utekelezaji wa mambo hayo matatu ni muhimu kwa kuwa tayari imebainika kuwa kuachana na matumizi ya nishati itokanayo na makaa ya mawe, ni miongoni mwa njia za msingi zaidi za kudhibiti ongezeko la kiwango cha joto duniani kisizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi.

"Hii ina maana uzalishaji umeme kwa kutumia makaa ya mawe lazima uwe chini ya asilimia 80 ya viwango vya mwaka 2010 ifikapo mwaka 2030. Zamani za kale makaa ya mawe yalileta umeme kwa gharama nafuu kwa maeneo mengi, na kuwa fursa ya ajira. Siku hizo zimepitwa na wakati. Zaidi ya nusu ya uwezo wa kuzalisha nishati jadidifu au salama ulioongezwa mwaka 2019 ulifanikisha upatikanaji umeme kwa gharama nafuu kuliko mitambo mipya ya makaa ya mawe. Nishati ya kisukuku inasababisha uchafuzi wa hewa na kuwa chanjo cha kifo cha mtu 1 kati ya 5 kila mwaka duniani kote.," amesema Katibu Mkuu.

Amekumbusha kuwa mkutano wa hivi majuzi kuelekea COP26 umeweka bayana kuwa mwelekeo wa kudhibiti ongezeko la joto duniani bado si mzuri kwa hiyo ni lazima kuchukua hatua za kijasiri.

Wanafunzi wakimsikiliza Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya msingi Mchoka akiwaelezea faida za mfumo wa maji unaosukumwa kwa nishati ya sola katika shule yao. Mradi huo umefanikishwa na UNICEF na wadau.
UNICEF/UN0372120
Wanafunzi wakimsikiliza Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya msingi Mchoka akiwaelezea faida za mfumo wa maji unaosukumwa kwa nishati ya sola katika shule yao. Mradi huo umefanikishwa na UNICEF na wadau.

IAEA na mbinu bunifu

Katibu Mkuu amesema gharama ya kuunda mtambo wa nishati salama ni nafuu kwa kuwa hata shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA, limebaini gharama nafuu ya ujenzi wa mtambo mpya wa sola kwa unafuu badala ya kutumia mtambo wa makaa yam awe.

"Nchini China na India, gharama za mtambo wa nishati salama inakuwa nafuu kila uchao. Hii leo natoa wito kwa serikali, kampuni binafsi na mamlaka za mitaa kuchukua hatua tatu," amesema Guterres.

Sitisheni miradi ya makaa ya mawe

Guterres anataka miradi mipya ya makaa ya mawe ikome na watu waache uraibu wa matumizi ya makaa ya mawe.

Achaneni na ufadhili wa makaa ya mawe

Katibu Mkuu anataka fedha za kuwekweza kwenye miradi ya makaa yam awe zielekezwe kwenye miradi mipya ya nishati rejelezi au salama asikie, "nasihi viongozi wa nchi zinazoongoza kwa kutoa hewa chafuzi zitangaze kuachana na usaidizi wao wa kimataifa ya makaa ya mawe mapema mwaka huu na usaidizi zaidi uelekezwe kwa nchi zinazoendelea ambazo zinajitahidi kutumia nishati salama kufikishia huduma wananchi wao."

Mpito kutoka makaa ya mawe kuelekea nishati salama

Katibu Mkuu anataka juhudi za pamoja za kuondoana na makaa ya mawe na kuelekea katika mitambo ya nishati salama akisema kipindi cha mpito kitakachotoa fursa ya kutoka mtambo mmoja hadi mwingine akisema "tafiti zimeonesha kuwa licha ya kwamba ajira zitapotea kwa kufungwa kwa mitambo, kipindi cha mpito kitawezesha kuzalishwa kwa mamilioni ya ajira ifikapo mwaka 2030."

Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utaunga mkono hatua za mpito na juhudi za kuhakikisha kuwa jamii zinazoingia kwenye marekebisho hayo zinachipuka na kustawi.