Dola milioni 266 zasakwa kunusuru wakimbizi Afrika Mashariki

2 Machi 2021

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasaka dola milioni 266 ili kunusuru wakimbizi milioni 3 waliokumbwa na mkato wa mgao kwenye nchi za Afrika Mashariki.

Mashirika hayo, lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la mpango wa chakula duniani, WFP, yametoa tangazo hilo leo kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa jijini Nairobi nchini Kenya,

"Uhaba wa fedha umelazimisha mashirika hayo kupunguza huduma zao kwa asilimia 60 na kuna hatari ya wakimbizi kukumbwa na ukosefu wa damu, utapiamlo na udumavu miongoni mwa watoto sambamba na hofu ya ukosefu wa usalama," imesema taarifa hiyo.

Madhara ya ukosefu wa fedha kwa familia za wakimbizi yanachochewa zaidi na vizuizi vya kutembea vinavyosababishwa na ugonjwa wa Corona au COVID-19 sambamba na hatua za kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, hali ambao tayari imekwamisha upatikanaji wa vyakula kwenye masoko yaliyoko kambini huku matumaini ya wakimbizi kusaidia familia zao kupitia vibarua na biashara ndogo ndogo yakizidi kuyoyoma.

Madhara ya makato ya mgao

Mkurugenzi wa ofisi ya UNHCR kanda ya Afrika Mashariki Clementina Nkweta-Salami anasema janga la Corona limekuwa na madhara makubwa lakini kwa wakimbizi, athari hasi ni maradufu.

Amesema "bila fedha za nyongeza kupatikana, maelfu ya wakimbizi wakiwemo watoto hawatakuwa na chakula cha kutosha. Hofu ya ukosefu wa ulinzi nayo inaongezeka, makato ya mgao wa chakula na fedha yanasababisha wakimbizi washindwe kumudu mahitaji yao ya lazima kama vile chakula, hivyo wanakula mlo mmoja, wanachukua mikopo kwa riba ya juu, wanauza mali zao, watoto wanatumikishwa, vile vile kuongezeka kwa matukio ya ukatili majumbani."

Kwa upande wake, Michael Dunford ambaye ni Mwakilishi wa WFP kanda ya Afrika Mashariki anasema ni lazima kuanza kukidhi mahitaji ya chakula na lishe kwa wakimbizi kwenye ukanda huo wa Afrika Mashariki hivi sasa.

"Kipaumbele chetu cha sasa ni kwamba lazima sote turejeshe angalau kiwango kidogo cha usaidizi kwa wakimbizi, wengi wao ambao wamepoteza mbinu za kjpatia kipato cha kutuma nyumbani kutokana na athari za COVID-19 duniani," amesema Bwana Dunford,

Anasema kuwa katu hawajawahi kuwa na kiwango cha chini cha fedha kama wakati huu, "tuna pengo la dola milioni 266 kwa kipindi cha miezi sita kijacho cha kukidhi mahitaij ya wakimbizi. Tuna hofu kubwa kuwa iwapo makato ya mgao yataendelea, wakimbizi watakumbwa na uchaguzi mgumu; kusalia kambini ambako chakula na hali ya usalama havitoshelezi au kurejea nyumbani ambako bado hali ya usalama si nzuri."

Katika nchi 11 zinazohudumiwa na UNHCR kanda ya Afrika Mashariki na pembe ya Afrika na Maziwa Makuu ,asilimia 72 ya wakimbizi milioni 4.2 wanakabiliwa na makato ya mgao wa chakula na misaada mingineyo.

Kwa upande wa WFP, uhaba wa fedha umesababisha kupunguza mgao wa kila mwezi kwa wakimbizi ambapo kwa Rwanda imepungua kwa asilimia 60, Uganda na Kenya asilimia 40, Sudan Kusini asilimia 30 na Djibout asilimia 23 ilhali Ethiopia mgao umepunguzwa kwa asilimia 16.

Ni wakimbizi nchini Burundi na Sudan pekee ambao wanapata mgao kamili na sasa dola milioni 18 zinahitajika kuwezesha huduma hiyo hadi mwezi Agosti mwaka huu.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter