Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nitatumia uzoefu, ujuzi na elimu yangu kuleta mabadiliko WTO: Ngozi Okonjo_Iweala

Dkt. Ngozi Okonjo-Iweala wa Nigeria, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirka la Biashara Duniani, WTO.
© WTO/Jay Louvion
Dkt. Ngozi Okonjo-Iweala wa Nigeria, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirka la Biashara Duniani, WTO.

Nitatumia uzoefu, ujuzi na elimu yangu kuleta mabadiliko WTO: Ngozi Okonjo_Iweala

Masuala ya UM

Mkurugenzi mkuu mpya wa saba wa shirika la biashara duniani WTO, Ngozi Okonjo-Iweala ameanza kazi rasmi Jumatatu akiwa ni mwanamke na Mwafrika wa kwanza kushika wadhifa huo na ameahidi kufanya kila awezalo kuleta mabadiliko.

Bi. Ngozi Okonjo akiwasili kwenye jengo la makao makuu ya WTO mjini Geneva Uswis kuanza rasmi kazi yake mpya akisema kuna kibarua  kikubwa cha kufanya na anahisi yuko tayari . 

Katika siku yake ya kwanza ofisini amekutana na wakurugenzi mbalimbali na wafanyakazi wengine wa shirika hilo  na kisha akaeekea kula kiapo na kutia saini ya kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na ipasavyo 

Siku hii imeghubikwa na shughuli nyingi ikiwemo kuhudhuria mkutano wa baraza la WTO kama mkurugenzi, baraza ambalo ndilo chombo cha juu kabisa cha kufanya maamuzi ya shirika hilo. 

Pamoja na kulishukuru baraza kwa kumuamini na kumuweka mamlakani, ameahidi kutumia uwezo wake wote, ikiwemo ujuzi, elimu na uzowefu wake kuleta mabadiliko. 

“Tunapaswa kuwajibika zaidi kwa watu tunaowahudumia. Tumekuja hapa kuhudumia , watu wa kawaida wanawake na wanaume na watoto wetu ambao wanatumai kwamba kazi yetu hapa ya kusaidia mfumo wa kimataifa wa biashara italeta mabadiliko ya kweli katika maisha yao, itaboresha hali ya maisha na kuunda ajira kwa wanaotafuta kufanya kazi.

Na katika zama hizi za janga la corona au COVID-19 ameliambia baraza hilo kwamba,“Tunahitaji kutoa kipaumbele katika hatua zetu dhidi ya COVID-19, zote zile za muda mfupi na za muda mrefu , na kujikita katika kukamilisha majadiliano ya ruzuku ya masuala ya uvuvi kabla ya katikati ya mwaka huu. Ni lazima tuafikiane mwelekeo kwa ajili ya mabadiliko ya mfumo wa kutatua migogoro na kuandaa mpango kazi wa kufikia lengo hili ambalo linaweza kuidhinishwa kwenye mkutano wa 12, MC12.” 

Mkutano huo wa 12 wa WTO katika ngazi ya mawaziri unatarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2021.  

Na kabla ya kukunja jamvi la siku ya kwanza kazini Bi. Ngozi Okonjo aalitembelea sanamu ya samaki iliyo karibu na lango kuu la WTO ambayo lengo lake ni kutoa ujumbe wa kukomesha ruzuku kwa uvuvi haramu na wito wa kukamilisha haraka majadiliano kuhusu ruzuku katika sekta ya uvuvi kabla hali haijawa mbaya zaidi.