WHO yapeleka mashine za Oksijeni Somaliland kuokoa maisha

Mtungi wa oxijeni wa kiafya
Samuel Ramos on Unsplash
Mtungi wa oxijeni wa kiafya

WHO yapeleka mashine za Oksijeni Somaliland kuokoa maisha

Afya

Vifaa vya oksijeni vilivyotolewa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO katika Hospitali Kuu ya Hargeisa huko Somaliland, si tu vinaleta tofauti kwa wagonjwa wa COVID-19 lakini pia watoto wenye homa ya mapafu na magonjwa mengine ya kupumua.

Ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, umeongeza mahitaji ya hewa ya oksijeni kwa ajili ya matibabu duniani na hivyo kufanya usambazaji wa vifaa vya oksijeni kuwa wenye umuhimu wa haraka zaidi. 

Mjini Hargeisa, mji mkuu wa Somaliland, katika pembe ya Afrika, wanaonekana wafanyakazi wa WHO wakiwa wamebeba makasha ya vifaa tiba tayari kwa usambazaji.  

Dkt Jamal Amran ni Mkuu wa ofisi ya WHO katika Somaliland anasema, "moja ya hatua za WHO ni kusaidia Somaliland na vifaa tiba vingi. Na mojawapo ya vifaa vikuu ni vya oksijeni.” 

Kwa mujibu wa WHO, inakadiriwa kuwa zaidi ya nusu milioni ya watu katika nchi za kipato cha chini na cha kati kwa sasa wanahitaji mitungi milioni 1.1 ya oksijeni kwa siku, na nchi 25 hivi sasa zinaripoti kuongezeka kwa mahitaji, nyingi zikiwa barani Afrika. Usambazaji vifaa tiba hivi ulikuwa unakwama hata kabla ya COVID-19 na hali imezidishwa zaidi na janga hilo. 

Wagonjwa wanaonekana katika Hospitali kuu ya Hargeisa, wakitumia vifaa hivi vilivyoletwa na WHO. Dkt Hamda Mamudin ni daktarin katika hospitali hii anasema,  "Upatikanaji wa sasa wa vifaa vya oksijeni, kwa mfano katika kituo chetu, hata baada ya janga la COVID-19 kumalizika, utasaidia kila mtoto aliye na homa ya mapafu, itasaidia kila mtu mzima mwenye  homa ya mapafu, itasaidia mtu mzima au mtoto yeyote na magonjwa yoyote ya kupumua ambayo yanahitaji oksijeni.  Vifaa hivi ni muhimu sana kwetu kwa havihitaji kujazwa kama mitungi ya oksijeni. Hivi vinahitaji umeme tu kufanya kazi vizuri.” 

Kuanzia mwezi Februari mwaka huu 2021, WHO na washirika wamesambaza zaidi ya vifaa vya Oksijeni 30,000  na vifaa vingine 40, 000  vya kufuatilia mwenendo wa hali ya mgonjwa katika nchini 121, zikiwemo nchi 37 ambazo zimeainishwa kuwa katika hali tete.