Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi zilizotolewa kwa ajili ya Yemen zakatisha tamaa- Guterres

Familia iliiyofurushwa kwao Taiz nchini Yemen ikiwa imepata hifadhi kwenye hema huko Fazal nchini Yemen.
UN OCHA/GILES CLARKE
Familia iliiyofurushwa kwao Taiz nchini Yemen ikiwa imepata hifadhi kwenye hema huko Fazal nchini Yemen.

Ahadi zilizotolewa kwa ajili ya Yemen zakatisha tamaa- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa umeelezea masikitiko yake kufuatia matokeo ya ahadi zilizotolewa katika mkutano wa kimataifa wa kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia Yemen mwaka huu wa 2021 ambayo inakabiliwa na janga la kibinadamu, linalotajwa kuwa kubwa zaidi duniani.  Makisio yalikuwa dola bilioni  3.85 lakini iliyopatikana ni takribani dola bilioni 1.7.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea masikitiko hayo kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake baada ya kutangazwa kuwa fedha zilizochangishwa leo kupitia mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao ni takribani dola bilioni 1.7 kiwango ambacho ni chini ya kile kilichopatikana kwenye mpango wa hatua kwa Yemen mwaka 2020.

"Kiwango cha leo ni pungufu kwa dola bilioni moja kulinganisha na ahadi zilizotolewa wakati wa mkutano wa kusaidia Yemen mwaka 2019," amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesema mamilioni ya watoto, wanawake na wanaume nchini Yemen wanahitaji msaada ili waweze kuishi. "Kupunguza msaada ni sawa na hukumu ya kifo. Kile kinachoweza kuelezewa kwa leo ni kama malipo ya awali. Nashukuru wale ambao wamejitolea kwa ukarimu na naomba wengine wafikirie tena kile wanachoweza kufanya ili kuondoa njaa ambayo dunia haijawahi kushuhudia kwa miongo kadhaa,"

Tweet URL

Suluhu ya Yemen si vita bali sitisho la mapigano

Guterres amesema njia pekee ya amani mara moja ni sitisho la mapigano nchini kote na kuweka mikakati ya kujengeana imani, ikifuatiwa na mchakato jumuishi wa kisiasa unaoongozwa na wayemen chini ya uratibu wa Umoja wa Mataifa ukiungwa mkono na jumuiya ya kimataifa akisema, "hakuna suluhisho lingine. Umoja wa Mataifa unaendelea kusimama kwa mshikamano na wananchi wa Yemen ambao wanakumbwa na njaa."

Mapema katika hotuba yake ya kufungua mkutano huo ulioandaliwa kwa pamoja na Uswisi na Sweden, Katibu Mkuu alielezea taswira ya kukatisha tamaa nchini Yemen akikumbusha kuwa njaa inasambaratisha Yemen ambako zaidi ya watu milioni 20 wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Takwimu hizo zinamaanisha kuwa watu wawili katika kila watu watatu nchini Yemen anahitaij msaada wa chakula, afya na huduma nyinginezo kutoka mashirika ya msaada.

Mwaka huu zaidi ya watu milioni 16 wanatarajiwa kukumbwa na njaa huku watu milioni nne wakiwa wamelazimika kukimbia makwao kutokana na mapigano.

Nchini Yemen mapigano mwaka jana pekee yalisababisa vifo na majeruhi zaidi ya 2,000, uchumi umetwama, huduma za umma halikadhalika huku janga la COVID-19 likiongeza ‘chumvi kwenye kidonda’.

Habari kwa Picha hii inakupatia taswira ya wanayopitia wayemen.