Mkuu wa OHCHR ataka uwazi na uchunguzi kufuatia kifo cha mwandishi mahabusu Bangladesh

1 Machi 2021

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo ametoa wito wa kuwepo na uwazi katika uchunguzi wa kifo cha mwandishi wa habari akiwa mahabusu nchini Bangladesh. 

Michelle Bachelet amesema mwandishi huyo Mushtaq Ahmed alikuwa mahabusuakishikiliwa kwa miezi tisa akisubiri kesi yake kwa kosa la kuchapisha Makala inayokosoa hatua za serikali za kupambana na janga la corona au COVID-19 na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii. 

Ahmed alifariki dunia tarehe 25 Februari baada ya kuhamishiwa kwenye hospitali ya magereza kwa ajili ya matibabu. 

Mamlaka nchini Bangladesh imetangaza kwamba itachunguza kifo chake kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR

“Serikali lazima ihakikishe kwamba uchunguzi wake dhidi ya kifo cha Ahmed ni wa haraka, wa uwazi na huru” amesisitiza Bi. Bachelet. 

Pia ameitaka mamlaka kufanya tathimini ya sheria ya usalama wa kidijitali ambayo ndio iliyotumika kumshitaki bwana ahmed, na ameitaka kusitisha kuitumia na kuwaachilia wote wanaoshikiliwa chini ya sheria hiyo kwa kutekeleza haki yao ya uhuru wa kujieleza na maoni. 

Bi. Bachelet ameongeza kuwa “Vyombo vingi vya haki za binadamu vimeelezea wasiwasi wao kuhusu sheria hiyo ya masuala ya usalama wa kidijitali ambayo imekuwa ikitumika kuwaadhibu wanaoikosoa serikali.” 

Ameelezea pia hofu yake kuhusu ripoti kwamba polisi wanadaiwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano ya kudai haki kwa kifo cha Ahmed huku kukiwa na ripoti kwamba watu 35 walijeruhiwa na saba kukamatwa. 

Watu kadhaa wamekamatwa 

Kamishina Mkuu ameelezea pia wasiwasi mkubwa kutokana na madai kwamba mwanaume mwingine anayekabiliwa na madai kama ya bwana ahmedmchora vikaragosi Ahmed Kishore ambaye yuko mahabusu amekuwa akikabiliwa na vitendo vya utesaji na ukatili mwingine. 

Bachelet ameikumbusha mamlaka nchini humo kuhusu wajibu wake wa kuchunguza haraka na kwa kina madai na kuhakikisha usalama na ustawi. 

Kwa mujibu wa OHCHR Bwana Ahmed na Bwana Kishore walikuwa ni miongoni mwa watu 11 waliokamatwa mwezi Mei mwaka jana kwa madai ya kusambaza taarifa potofu kuhusu COVID-19 au kukosoa hatua za serikali za kupambana na ugonjwa huo. 

“Watu hao wamenyimwa dhamana mara nyingi na walisalia rumande wakisubiri kesi zao kwa miezi tisa kabla hawajashitakiwa rasmi tarehe 20 Januari mwaka huu kwa kuchapisha “propaganda, taarifa za uongo au kukosoa na taarifa ambazo zinaweza kuvuruga utulivu na kusababisha machafuko.” 

Wiki iliyopita Jumanne walifikishwa mahakamani ambapo bwana Kishore alidaiwa kwamba aliteswa na maafisa wa polisi na kwa mujibu wa duru za Habari alionekana ameumia. 

Madai ya ukatili ni mtihani 

Ofisi hiyo ya haki za binadamu imesema madai ya vitendo vya ukatili na utesaji vinavyodfanywa na vikosi vya usalama vya kuchukua hatua za dharura limekuwa ni suala linalotia hofu kwa muda mrefu sasa. 

Kamati ya kupinga utesaji ambacho ni chombo huru kinachofuatilia utekelezaji wa mkataba dhidi ya utesaji na vitendo vingine vya kikatili , kudhalilisha haki za binadamu au kuadhibu, mwaka 2019 ilipendekeza kwa serikali ya Bangladesh kufanya uchunguzi hudu dhidi ya madai kwamba askari wa vikosi hivyo maalumu wanatekelreza vitendo vya utesaji na ukiukwaji mwingine wa haki ikiwemo kukamata watu kiholela, watu kutoweshwa na mauaji ya kinyume kinyume cha sheria. 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter