Katibu Mkuu wa UN alaani vikali ukandamizaji nchini Myanmar. 

28 Februari 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, analaani vikali ukandamizaji nchini Mynmar, imeeleza taarifa iliyotolewa hii leo Jumapili kupitia msemaji wake mjini New York, Marekani.  

“Katibu Mkuu Guterres anasikitishwa sana na ongezeko la vifo na majeraha mabaya. Matumizi ya nguvu iliyopitiliza dhidi ya wanaoandamana kwa amani na kukamatwa kiholela, haikubaliki.” Imesema taarifa.  

Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa Katibu Mkuu anahimiza jamii ya kimataifa kushirikiana na kutuma ishara ya wazi kwa jeshi kwamba lazima liheshimu mapenzi ya watu wa Myanmar kama ilivyooneshwa kupitia uchaguzi na kuacha ukandamizaji. 

OHCHR nayo yatoa tamko 

Na katika kukemea yanayoendelea nchini Myanmar, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR nayo hii leo Jumapili imelaani vikali ghasia zinazozidi nchini humo na kutaka kukomeshwa mara moja matumizi ya nguvu ambayo hadi taarifa hizi zinatolewa, waandamanaji wasiopungua 18 walioandamana dhidi ya mapinduzi ya kijeshi ya Myanmar wamepoteza maisha.  

Kwa mujibu wa OHCHR, katika kile walichokiita “habari za kuaminika”, zaidi ya waandamanaji 30 wamejeruhiwa wakati polisi na vikosi vya kijeshi vilipotumia risasi za moto moja kwa moja kuelekea katika umati wa watu na nguvu ya kupindukia.  

"Watu wa Myanmar wana haki ya kukusanyika kwa amani na kudai kurejeshwa kwa demokrasia." amesema msemaji wa OHCHR, Ravina Shamdasani. 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter