Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Côte d'Ivoire yawa ya pili Afrika kupokea chanjo kupitia COVAX

Shehena ya dozi 504,000 za chanjo dhidi ya COVID-19 zikiwasili nchini Côte d'Ivoire.
© UNICEF/Milequem Diarassouba
Shehena ya dozi 504,000 za chanjo dhidi ya COVID-19 zikiwasili nchini Côte d'Ivoire.

Côte d'Ivoire yawa ya pili Afrika kupokea chanjo kupitia COVAX

Afya

Côte d'Ivoire imekuwa nchi ya pili baada ya Ghana, kupokea dozi za chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 kupitia mfumo wa kimataifa wa COVAX wa kusaka na kusambaza chanjo hizo kwa nchi za kipato cha chini na kati.
 

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF iliyotolewa leo  mji mkuu wa kibiashara wa Côte d'Ivoire, Abidjan, imesema, COVAX imepeleka shehena ya dozi 504,000 ya chanjo aina ya AstraZeneca/Oxford iliyotengenzwa na taasisi ya Serum nchini India.

Sambamba na dozi ni pamoja na mabomba 505,000 ya sindano na shehena hiyo ni sehemu ya mpango wa COAX wa kusambaza dozi angalau bilioni 2 kwa nchi za kipato cha kati na chini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2021.

Chanjo hizo zimepokelewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abidjan na Waziri wa Afya wa Côte d'Ivoire Dkt. Eugène Aka Aouélé, akiwa ameambatana na wawakilishi wa taasisi zinazounda COVAX ambazo ni fuko la chanjo duniani, GAVI, UNICEF, WHO, CEPI na Muungano wa Ulaya, miongoni mwa wachache.

Tweet URL

Fedha kutoka wadau hao zimewezesha kutengenezwa, kusafirishwa na kusambazwa kwa chanjo hizo.

Chanjo zimesafirishwa kutoka Mumbai India kupitia Dubai Falme za kiarabu ambako mabomba ya sindano yanayohifadhiwa kwenye bohari mjini Dubai yaliunganishwa kwenye shehena ya chanjo.

Akizungumzia shehena hiyo baada ya kuwasili, Waziri wa Afya wa Côte d'Ivoire amesema wamefurahi na kwamba ni hatua muhimu katika vita vya pamoja dhidi ya adui Corona.

Amesema janga la Corona limesababisha vifo vya mamilioni duniani ambapo Côte d'Ivoire pekee watu 188 wamefariki dunia kwa Corona kati ya wagonjwa zaidi ya 32,000.

Naye mwakilishi wa UNICEF nchini humo Marc Vincent amesema chanjo huokoa maisha. “Jinsi wafanyakazi wa afya na wengine walio mstari wa mbele wanapatiwa chanjo, tutaona hali ya kawaida inarejea taratibu, ikiwemo kuimarika kwa huduma za afya, elimu na huduma nyingine hususan kwa watoto. UNICEF na wadau wake wanashirikiana kusaidia nchi kujiandaa ili kuanza kutoa chanjo dhidi ya COVID-19 na kuzindua tena kampeni za chanjo.”