Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC yazindua dira ya Afrika kukabili uhalifu na madawa ya kulevya ifikapo mwaka 2030

Hakuna nchi au eneo ambalo haliwezi kukabiliwa na ufisadi, changamoto ambayo inakwamisha maendeleo.
Picha: UNODC
Hakuna nchi au eneo ambalo haliwezi kukabiliwa na ufisadi, changamoto ambayo inakwamisha maendeleo.

UNODC yazindua dira ya Afrika kukabili uhalifu na madawa ya kulevya ifikapo mwaka 2030

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabili uhalifu na madawa ya kulevya, UNODC, Ghada Waly amezindua dira ya mkakati wa Afrika kwa mwaka 2030, uzinduzi uliofanyika kimtandao hii leo wakati wa mkutano wa ngazi ya juu.  

Mkakati huo wa miaka 10 unalenga kupatia nchi za Afrika njia bunifu za kuimarisha uwezo wa kuzuia uhalifu, kuimarisha utendaji wa mifumo ya haki, kukabiliana na uhalifu  wa kupangwa, ufisadi,  madawa ya kulevya na utawala wa sheria wakati huu ambapo nchi zinahaha kukabiliana na COVID-19.  

Bi Waly amesema, “mkakati wetu wenye maono unawakilisha mbinu tofauti ya kuleta mabadiliko katika kazi zetu na unalenga kuchukua muundo jumuishi, unaojali watu na unaozingatia haki za binadamu kwa ajili ya kuimarisha jamii za kiafrika kukabiliana na madawa na uhalifu.”

Wakati UNODC ikilenga kuchukua muundo wa aina hiyo inatambua changamoto zinazokabili takriban watu milioni 489 wanaoishi katika umasikini. Aidha janga la virusi vya corona au COVID-19 limeongrza ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto kwa ujumla na limeongeza idadi ya wahamiaji wanaosafirishwa kiharamu, wakimbizi na watoto na barubaru, idadi ya watu kwenye jela na watu wanaotumia madawa ya kulevya.
UNODC imesema ufisadi na ukosefu wa uwajibikaji na mbinu za ufuatiliaji vinaathiri maendeleo endelevu barani Afrika, usalama wa binadamu na usimamizi. Waafrika wananyimwa zaidi ya dola bilioni 50 kila mwaka ya pesa za umma na binafsi ambazo zinapatikanakwa njia haramu, zinahamishwa au kutumiwa visivyo kwa mujibu wa ripoti ya Mbeki kuhusu uhamishaji haramu wa fedha. Takriban dola bilioni 88.6 sawa na asimia 3.7 ya pato la Afrika, husafirishwa nje kila mwaka.
Ikiwa ni chini ya miaka kumi tangu kufika ukomo wa malengo ya maendeleo endelevu, mkakati wa UNODC kwa Afrika unaweka njia kuwezesha wadau kusaidia katika kuzindua nguvu na raslimali zake kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hizo. Bi. Waly amesema, “kwa kuwajengea mnepo na kuimarisha mfumo wa sheria, tunaweza kusaidia nchi za Afrika kufikia maono yao kwa ajili ya maendeleo endelevu.”