Nchi kadhaa zinazoendelea zinafanya vizuri katika matumizi ya teknolojia mpya lakini nyingi zasalia nyuma-UNCTAD Ripoti 

25 Februari 2021

Baadhi ya mataifa yanayoendelea yanaonesha uwezo wa kutumia na kuchukua teknolojia mpya ikilinganishwa na vipimo vya pato la kitaifa lakini nyingi bado zinasalia nyuma, imesema ripoti mpya ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD ya mwaka 2021 ambayo imetolewa leo Februari 25 mjini Geneva Uswisi. 

Teknolojia hizo mpya ni zile ambazo zinatumia maendeleo ya dijitali na utandawazi ikiwemo akili bandia, mtandao wa kizazi cha sasa wa 5G uchapishaji kutumia bapa tatu au 3D, ndege zisizo na rubani na nyinginezo.  

UNCTAD imesema teknolojia hizi zinazindua dunia mpya hususan hali baada ya janga la corona au COVID19.

Aidha licha ya athari mbaya itokanayo na matumizi ya teknolojia hizo kama vile kupanua pengo la ukosefu wa usawa na kupanua pengo la kidijitali na kusambaratisha umoja wa kijamii na kisiasa huenda zikaleta mabadiliko na kusaidia katika kufikia melengo ya maendeleo endelevu. 

Ripoti imetoa takwimu kuhusu utayari wa nchi katika kutumia teknolojia hizo mpya kwa kuzingatia  uwezo wao wa kitaifa unaohusiana na uwekezaji, nguvu kazi na juhudi za teknolojia. Inapima utayari wa nchi kutumia teknolojia hizo kwa kuzingatia mambo matano: usambazaji wa  teknolojia ya habari na mawasiliano, ujuzi, utafiti na maendeleo, shughuli za viwanda na uwezo wa kufikia ufadhili. 

Moja ya nchi zinazofanya vizuri ikilinganishwa na pato lao la kitaifa ni India ikifuatiwa na Ufilipino 

Kwa ujumla hata hivyo nchi tano zilizoendelea za kwanza zinazofanya vizuri zina viwango vya chini vya mtandao wa teknolojia ya habari na mawasiliano na ujuzi na hili limejitokeza kwa mataifa yaliyoendelea kwa ujumla. 

Nchi kama Marekani, Uswisi na Uingereza zimetajwa kuwa zimejiandaa vizuri kwa ajili ya matumizi ya teknolojia mpya.

  UNCTAD imetoa wito kwa mataifa yanayoendelea kukumbatia teknolojia mpya wakati yakiendelea kupanua uzalishaji kwa kuzijua teknolojia zilizopo kwa sasa. 

Ripoti imeongeza kwamba nchi hizo zinahitaji kuimarisha mifumo yao ya ubunifu kwani nyingi ni dhaifu na ziko hatarini ya kukumbwa na hitilafu ya mifumo na upungufu wa vifaa. 

Ripoti imetoa wito kwa serikali kushirikisha wadau mbali mbali ambao wanaweza kuleta uwiano kati ya sayensi teknolojia na ubunifu na sera nyingine za kiuchumi. 

Halikadhalika  watunga sera wasaidie watu kupata stadi za kidijitali na ujuzi kwa ajili ya kukumbatia teknolojia mpya katika uzalishaji nchini mwao. 

Aidha UNCTAD kupitia ripoti imesema serikali zinapaswa kuhakikisha kila mtu yupo mtandaoni kwa kuwapa kipaumbele walio nyuma zaidi kwani teknolojia mpya zinahitaji ukuaji wa kidijitali na utandawazi. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter