Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ingawa Corona ilininyima masomo na kunipora miguu yangu, haitopokonya ndoto yangu: mtoto Chirstine 

Barubaru akisoma nyumbani wakati wa COVID-19 nchini Uganda
© UNICEF/Francis Emorut
Barubaru akisoma nyumbani wakati wa COVID-19 nchini Uganda

Ingawa Corona ilininyima masomo na kunipora miguu yangu, haitopokonya ndoto yangu: mtoto Chirstine 

Afya

Kutana na binti kutoka Uganda, Christine Joyce ambaye anasema asilani hatolisahau janga la corona au COVID-19 ambalo mbali ya kumnyima masomo wakati wa sheria za kusalia majumbani limechangia kumwacha na kilema cha maisha. Hata hivyo amesema hatokata tamaa ya kutimiza ndoto yake ya kuendelea na masomo na hatimaye siku moja kuwa daktari.

Christine Joyce mwenye umri wa miaka 15 ni mkazi wa Kampala nchini Uganda na sasa ana ulemavu wa kutokuwa na miguu yote miwili na anatumia kitimwendo.

 Anasoma shule ya msingi  na baada ya kuamka, kujitayarisha na kupata kifungua kinywa anavalia sare ya shule na barakoa yake tayari kwenda shule na kaka yake anayemsaidia kumsukuma kwenye kiti mwendo. 

Kama walivyo mamilioni ya wanafunzi wengine kote duniani amefurahi sana shule zilipofunguliwa tena baada ya muda mrefu wa kusalia majumbani. “Nilijisikia vizuri sana kujua kwamba ninarejea shuleni, kwa sababu nilikuwa nausubiria wakati huu kwa muda mrefu sana. Nahisi niko salama shuleni kwa sababu waalimu wetu wanachukulia hatua za kujikinga na COVID-19 kwa umuhimu mkubwa” 

Pamoja na furaha kubwa aliyonayo kurejea shuleni Christine anakabiliwa na changamoto kutokana na ulemavu alionao. “Shule yangu haikujengwa na mazingira ya kuruhusu kiti mwendo, hivyo napata changamoto kubwa ya kutoka sehemu moja hadi nyingine. Lakini ni muhimu kwangu kuendelea kuja shuleni kwa sababu napata fursa ya kuchangamana na waalimu uso kwa uso na kuwaauliza maswali ambapo sielewi.” 

Kabla ya janga la COVID-19 Christine alikuwa na miguu yake yote miwili , hadi pale ajali ilipomfika wakati wa sheria za kusalia majumbani kutokana na corona,“Jumatatu moja jioni mwezi Julai mama alitutuma mjini kununua ndala na hapo ndipo gari lilikuja na kutugonga barabarani, nilipoteza miguu yangu yote miwili na nililazwa hospitali kwa miezi mitatu. Naamini kila kitu kinatokea kwa sababu fulani.” 

Akiwa hospitali alishuhudia upungufu mkubwa wa madaktari na Christine akapata motisha “Nikaamua kurudi shuleni kwa sababu ndoto yangu ni kuwa daktarin na njia pekee ya kuwa daktarin ni kuendelea na masomo.”