Skip to main content

Kujikwamua na COVID-19 ni fursa ya kuhakikisha haki za binadamu kwa wote:Guterres

Mtaa wa Camuna 13 kwenye mji wa Medellin Colombia
IMF/Joaquin Sarmiento
Mtaa wa Camuna 13 kwenye mji wa Medellin Colombia

Kujikwamua na COVID-19 ni fursa ya kuhakikisha haki za binadamu kwa wote:Guterres

Haki za binadamu

Haki za binadamu zimeathirika vibaya wakati wa janga la corona au COVID-19, lakini wakati huu wa kujikwamua na janga hilo ni fursa muhimu ya kuboresha hilo na kuhakikisha utu kwa wote, amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwenye Baraza Kuu la Umoja huo.

Guterres ameyasema hayo mbele ya mabalozi ikiwa ni mwaka mmoja kamili tangu alipotoa wito wa kimataifa wa kuchukua hatua kuhusu haki za binadamu, wito uliojumuisha vipengele 7 vyenye lengo la kuboresha hali ya usawa na kupunguza madhila kila mahali.

Kukiwa na changamoto za kupiunguzwa kwa bajeti na mgogoro wa kifedha Katibu Mkuu aliomba msaada kwenye ofisi ya kamishina mkuu wa haki za binadamu OHCHR, na vyombo vingine husika akitambua kwamba ufadhili ni muhimu katika kufikia mabadiliko ya kweli.

“Kama ilivyo kwa chanjo ya COVID-19, haki za binadamu hazitoweza kutupeleka kwenye dunia yenye afya bora endapo zitapatikana tu kwa wachache wanaojiweza.” Ameonya bwana Guterres.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
UN Photo/Violaine Martin (file)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

COVID-19 imeanika pengo la usawa

Katibu Mkuu alizindia wito wa kuchukua hatua wiki chache tu kabla ya kutangazwa kwa janga la COVID-19, janga kubwa kabisa kwa vizazi kadhaa ambalo limeanika pengo kubwa la usawa, ubaguzi , hasa kwa wanawake,walio wachache, wazee na watu wenye ulemavu miongoni mwa walioathirika zaidi.

Wakati huohuo mifumo ya haki na ulinzi imejaribiwa, kudhoofishwa n ahata kusambaratishwa nah atua za dharura wakati wa janga la COVID-19 zikuwa zikitumika kama hata kubinya au kuharamisha uhuru wa msingi amesema Katibu Mkuu na kuongeza kwamba 

“Katika kujijenga upya kwa pamoja tuna fursa ya kipekee nay a kihistoria kujenga dunia mbayo kila mtu anathaminiwa utu wake, ambayo kila jamii inaweza kumudu majanga, ambayo mustakbali wa kila mtu unajengwa katika misingi ya haki zisizopingika.”

Rais wa Baraza Kuu

Naye Rais wa Baraza Kuu Volkan Boskir amesisitiza kwamba mtazamo wa haki za binadamu kila wakati ndio mtazamo sahihi, iwe ni katika zama za migogoro, vita, amani na majanga.

Volkan Bozkir, Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu
UN Photo/Loey Felipe
Volkan Bozkir, Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu

“Hatua zote za kukabiliana na janga la COVID-19 lazima ziwekwe kwa kuheshimu haki za binadamu.”

Ameongeza kuwa “Wadau wote wanahitaji kushiriki katika kufanya maamuzi na kutoa tathimini ili tuweze kubaini, ni nani aliyeathirika zaidi, kwa nini hayo yametokea na jinsi gani tunaweza kuwalinda watu binafsi na jamii sasa na wakati tutakapokabiliwa na changamoto nyingine ya kimataifa.”

Haki za binadami ni kitovu cha hatua

Haki za binadamu ni kipaumbele cha juu cha watu duniani kwa mujibu wa utafiti wa kimataifa ulifanywa mwaka jana katika kuadhimisha miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, amesema Katibu Mkuu.

“Kwa msaada wenu mwaka jana , wito wa kuchukua hatua unaadhimisha mafanikio. Familia ya Umoja wa Mataifa inashirikiana kuhakikisha kwamba haki za binadamu zinakuwa kitovu cha mipango ya kiuchumi na kijamii ya kujikwamua na COVID-19.”

Umoja wa Mataifa umetoa matamko mbalimbali ya kisera ambayo yanaainisha kwamba hatua katika maeneo muhimu ambayo yanajumuisha mtazamo wa haki za binadamu au katika kufuta sheria zilizopitwa na wakati ambazo zinabagua dhidi ya wanawake.