Pamoja na magumu wanayopitia, raia wa DRC waonesha mshikamano

24 Februari 2021

Ikiwa leo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA inapatia nchi wanachama wa Umoja huo hali halisi ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, , raia nchini humo licha ya machungu wanayopitia na madhila yanayowakabili  wameendelea kuonesha mshikamano wa ajabu baina yao ili angalau kupunguza machungu wakati jamii ya kimataifa ikihana kuwanusuru.

Pembezoni kidogo ya msitu mkubwa, katika eneo la Kalunguta, Jimboni Kivu kaskazini, Bwana Katembo na wenzake wanashirikiana kujenga nyumba ya miti katika eneo walilopewa na waenyeji.  

"Sikujua waliokuwa wanagombana ni akina nani. Watu wengi waliuawa. Ndio maana tutakimbilia huku.

Katembo aliyakimbia makazi yake bila chochote. Akiwa amefurushwa yeye na familia yake, analazimika kujenga maisha mapya. Kwa kushirikiana, wanajengeana nyumba, na leo ni zamu yake Katembo, "Tuliteseka. Hakuna chakula. Pa kulala hakuna. Lakini watu hapa wanaonesha mshikamanowanatusaidia sisi wakimbizi. Hata wametupatia ardhi kwa ajili ya ujenzi ili tuwe salama. Tuko watu kumi kutoka eneo moja, tunasaidiana. Tunamaliza nyumba ya mmoja, kisha tunahamia kwa mwingine, na mwingine na mwingine, hivi hivi. Leo tunajenga nyumba yangu."  

Jeannine ni mjane ambaye analea watoto wake nane. Anawekeza nguvu zake zote kwao kwa ajili ya maisha yao ya baadaye, anasema, "Bado nina matumaini kuwa siku moja, ninaweza kurudi nilikotoka. Lakini sasa sina nyumba tena. Mama yangu alishakufa. Mume wangu pia. Nilikuwa nashindwa kukimbia na watoto. Watoto wanacheka, wanacheza. Hawaoneshi huzuni sana. Wanashukuru kwa kila siku mpya. Mimi napenda wasome ili wawe na maisha bora. Watoto wawapende wanaowakuta pale, . Hayo ndiyo maisha ninayowatakia. Lakini sasa ni vigumu kupata chakula cha kuwalisha. Nitawasomesha namna gani?

Kwa mujibu wa OCHA, inadakadiriwa kuwa katika mwaka huu wa 2021, kufikia watu milioni 19.6, watahitaji msaada wa kibindamu nchini DRC.  

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter