Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la Corona lapeleka mrama mgao wa vyakula shuleni- WFP 

Mlo shuleni ni muhimu hususan kwa watoto maskinia
WFP/Sierra Leone
Mlo shuleni ni muhimu hususan kwa watoto maskinia

Janga la Corona lapeleka mrama mgao wa vyakula shuleni- WFP 

Msaada wa Kibinadamu

Mafanikio ya miongo kadha ya mgao wa chakula shuleni yaliyolenga watoto walio hatarini na wasio na uwezo wa kupata mlo bora, yako hatarini kutumbukia nyongo kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa hii leo huko Roma Italia ikimulika hali ya mpango wa mlo shuleni duniai, SOSFW

Ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP, imesema mtoto mmoja kati ya wawili sawa na watoto milioni 388 duniani kote walikuwa wanapata mlo kila siku wakati janga la COVID-19 lilipoanza, idadi ambayo ni ya kihistoria kuwahi kufikiwa. 

Hata hivyo ujio wa Corona ulibadili mwelekeo kwa kuwa “ilipofika mwezi Aprili mwaka 2020, nchi 199 zilifunga shule na watoto milioni 370 walinyimwa ghafla kile ambacho walikuwa wanapatiwa kila siku mlo wenye lishe bora.” 

Ripoti hiyo imesema  “kwa serikali, zuio la kutembea lilimulika dhima muhimu ya mpango wa mlo shuleni katika kusaidia watoto walio hatarini zaidi  na kuwalinda kwa mustakabali wao .” 

Ni kwa mantiki hiyo ripoti inataka hatua za dharura kurejesha huduma hiyo kama ilivyokuwa inatolewa kabla ya COVID-19 na kupanua zaidi ili kufikia watoto wengine milioni 73 ambao walikuwa hawafikiwi na mpango wa mlo shuleni kabla janga la Corona kuibuka. 

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, David Beasley amesema “mpango wa mgao wa mlo shuleni umeleta mabadiliko makubwa . Huo mlo mmoja kwa siku ni sababu kwa watoto wenye njaa kutaka kwenda shuleni. Halikadhalika ni kichocheo kizuri cha kuhakikisha watarejea shuleni hata vizuizi vya kufungwa shule vitakapoondolewa. Tunahitaji programu kama hizi zianze tena na ziwe bora zaidi kuliwa awali na hatimaye tuondokane na COVID-19 kuvuruga mustakabali wa mamilioni ya watoto walio hatarini sehemu mbalimbali duniani.” 

Mwaka 2021, WFP imesema itajenga ubia kusaidia serikali kuimarisha mipango ya mgao wa mlo shuleni, ambapo shirika hilo litashirikiana na mashirika ya maendeleo. Wahisani, sekta binafsi na mashirika ya kiraia. 

Kati yam waka 2013 na 2020, idadi ya watoto wanaopata mlo shuleni iliongezeka duniani kote kwa asilimia 9 na katika nchi nchi za kipato cha chini ongezeko lilikuwa asilimia 36, kwa kuwa serikali zilipanua wigo wa miradi hiyo na kufanya mgao wa chakula shuleni kuwa mradi wa wa kina zaidi wa hifadhi ya kijamii duniani. 

Watoto nchini India wakipata mlo shuleni kama sehemu ya mpango wa WFP
WFP/Isheeta Sumra
Watoto nchini India wakipata mlo shuleni kama sehemu ya mpango wa WFP

 

Tafiti za umuhimu wa mlo shuleni kwa mustakabali wa mtoto 

Tafiti zimeonesha kuwa kwa maisha ya mtoto kutoka familia maskini, mlo shuleni unaweza kuwa na mchango mkubwa. Mlo huo unaepusha njaa , unasaidia kujenga afya yake kwa muda mrefu na kusaidia mtoto kujifunza na kustawi.  

Kwa watoto wa kike manufaa hayo ni dhahiri zaidi kwenye maeneo ambako kuna mlo shuleni kwa kuwa wanabakia shuleni muda mrefu, viwango vya ndoa katika umri mdogo vinapungua halikadhalika ujauzito katika umri mdogo. 

Vyakula vinavyolimwa na jamii huchochea uchumi wa jamii 

Ripoti ya WFP inasema kuwa mpango wa mlo shuleni unapotumia mazao yaliyolimwa kwenye jamii husika huchochea uchumi wa jamii. “Huongeza mahitaji ya milo tofauti, mlo wenye lishe na kuweka hakikisho la soko na kusaidia kilimo cha eneo husika na kuimarisha mifumo ya chakula ya jamii.” 

Ripoti inaenda mbali zaidi ikieleza kuwa mipango ya mlo shuleni inaleta faida kubwa ya had idola 9 kwa kila dola 1 inayowekezwa kwenye mradi huo. Halikadhalika huotoa fursa ya ajira ambapo kwa mujibu wa WFP ajira mpya 1,668 huanzishwa kwa kila watoto 100,000 wanaolishwa chakula shuleni. 

Ni kwa mantiki hiyo Beasleay anasema, “WFP imejizatiti kushirikiana na wadau kuhakikisha hakuna mtoot, bila kujali anakoishi, anakuwa na njaa shuleni au mbaya zaidi haendi shuleni kabisa. Baada ya janga la miezi ya sasa, lazima tutumie fursa iliyopo kujenga dunia bora zaidi ambayo wote tunataka kuiona.”