Ukuaji wa haraka wa uchumi wa kidijitali unahitaji majibu madhubuti ya sera

23 Februari 2021

Ripoti mpya ya shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, ILO iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi, imesema majukwaa ya kazi ya kidijitali ulimwenguni yameongezeka mara tano katika muongo mmoja uliopita ingawa kunahitajika utatuzi wa adha zinazoambatana na ukuaji huo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ILO ya Ajira Ulimwenguni na Mtazamo wa Kijamii mwaka 2021, Jukumu la majukwaa ya kazi ya kidijitali katika kubadilisha ulimwengu wa kazi, majukwaa ya kazi ya kidijitali yanatoa fursa mpya za kazi, yakijumuisha wanawake, watu wenye ulemavu, vijana na wale waliotengwa katika masoko ya jadi ya kazi. Majukwaa pia yanaruhusu biashara kupata nguvu kazi kubwa yenye ujuzi tofautitofauti huku wakipanua wigo wa wateja wao.  

Ripoti hiyo iliyowahoji wafanyakazi 12, 000 na wawakilishi wa makampuni ya biashara 85 kote ulimwenguni katika sekta mbalimbali, inazingatia aina mbili kuu za jukwaa la wafanyakazi wa kidijitali, yaani majukwaa ya wavuti mtandaonii, ambapo kazi zinafanywa mtandaoni na nje ya ofisi, na majukwaa yale ambayo yanamtraka mfanyakazi kuwa mahali fulani, mfano madereva wa teksi, na wasambazaji wa huduma.   

Ripoti inasema kuna changamoto mpya kwa wafanyakazi na biashara ambapo changamoto kwa wafanyakazi wa mtandaoni zinahusiana na hali za ufanyaji kazi, mapato, na ukosefu wa upatikanaji wa ulinzi wa jamii, uhuru wa kujumuika na haki za kujadiliana kwa pamoja. Saa za kufanya kazi zinaweza kuwa ndefu na zisizotabirika. Nusu ya wafanyakazi wa jukwaa mtandaoni wanapata chini ya dola 2 za Marekani kwa saa, ripoti inaeleza.  kwa saa. Pia majukwaa mengine yana mapengo makubwa katika suala la kijinsia. Janga la COVID-19 limefunua zaidi masuala haya, ripoti hiyo imeendelea kufafanua.  

MkurugeNzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder anasema, "majukwaa ya kazi ya kidijitali yanafungua fursa ambazo hazikuwepo hapo awali, haswa kwa wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na vikundi vilivyotengwa katika sehemu zote za ulimwengu. Hiyo lazima ikaribishwe. Changamoto mpya zinazoletwa na hali hiyo zinaweza kukabiliwa kupitia mazungumzo ya kijamii ulimwenguni ili wafanyakazi, waajiri na serikali waweze kufaidika kikamilifu na kwa usawa na maendeleo haya. Wafanyakazi wote, bila kujali hali ya ajira, wanahitaji kuweza kutumia haki zao za msingi kazini.” 

Aidha ripoti imeeleza kuwa gharama na faida za majukwaa ya kidijitali hayana mgawanyo sawa ulimwenguni kote. Kwamba asilimia tisini na sita ya uwekezaji katika majukwaa kama haya yamejilimbikizia Asia, Amerika Kaskazini na Ulaya. Asilimia sabini ya mapato yamejikusanya katika nchi mbili tu, Marekani na China. 

Vilevile ripoti hiyo imefafanua kuwa biashara zinatafuta majukwaa ya kidijitali katika nchi zilizoendelea, huku wanaofanya kazi wakiwa katika ulimwengu wa nchi za kipato cha chini na pia ujira kati ya makundi hayo mawili hutofautiana bila kuzingatia usawa. 

Ripoti hiyo ya ILO imeshauri kuwa, kwa kuwa majukwaa ya wafanyakazi wa kidijitali hufanya kazi katika mamlaka nyingi, mazungumzo ya sera ya kimataifa na uratibu inahitajika ili kuhakikisha uhakika wa udhibiti na utekelezwaji wa viwango vya kazi vya kimataifa. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter