Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afurushwa kwao Ituri, DRC mara tatu sasa amekata tamaa ya kurejea nyumbani 

Charlotte (kushoto) na Françoise  (kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Loda jimboni Ituri nchini DR Congo.
© UNICEF/UN0381753/Roger LeMoyne
Charlotte (kushoto) na Françoise (kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Loda jimboni Ituri nchini DR Congo.

Afurushwa kwao Ituri, DRC mara tatu sasa amekata tamaa ya kurejea nyumbani 

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kikongwe anayelea wajukuu wake baada ya mtoto wake kuuawa kwenye mapigano amekata tamaa ya maisha akisema hana matumaini yoyote na anahofia kuwa akirejea nyumbani atauawa.

Nyakati za asubuhi jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,  DRC, Anasthasia Chove mwenye umri wa miaka 72 akielekea shambani na wajukuu zake. 

Nats 

Baada ya kukwatua shamba lao sasa safari ya kurejea nyumbani wakiwa na mavuno ambayo ni mboga ya kabichi na mahindi. 

Nats.. 

Anasthasia anaishi kambini Ituri akisema hii ni mara ya tatu anakimbia nyumbani wake na kuhamia hapa. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2003, kisha 2017 na mwaka jana 2020. 

Nats.. 

Anastazia akipukuchua mahindi kutoka shambani akiwa na wajukuu zake anasema wanamgambo walifika kijijini kwetu na kuanza kushambulia kwa risasi kwa haraka sana kiasi kwamba hatukufahamu pa kukimbilia. Mwanangu wa kiume aliuawa. Hivi sasa ninalea watoto wake wanne. Mkubwa ana umri wa miaka 15. Wengine ni miaka 12, minane na mitano.” 

Hugo Kambale ni mtaalamu wa masuala ya dharura kambini hapa Ituri kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF. “Mzozo huu chanzo chake ni jamii na wanapigania ardhi. Tumekuwa na awamu tatu za ghasia ambazo zimesababisha watu kukimbia makwao. Kuna ukatili, watu wanauawa, vijiji vinateketezwa, mali zinaharibiwa, huduma za msingi kama shule, afya zimesambaratishwa na vikundi vyenye silaha.” 

Idadi kubwa ya wakimbizi hapa ni wanawake na watoto ambapo Hugo anasema tangu mzozo uanze wamechukua hatua kuleta huduma za msingi kama vyoo, maeneo ya watu kuoga na pia vituo vya kupata maji safi na salama. 

Halikadhalika kuna vituo salama kwa watoto kucheza na kupata huduma za ushauri nasaha na kisaikolojia. 

Kwa Anastasia, suala la kurejea nyumbani bado ni ndoto. 

“Kama amani ingalikuwepo, ningalirejea nyumbani, lakini si sasa, hilo haliwezekani. Iwapo nitaenda nyumbani sasa, nitauawa kwa sababu wanamgambo bado wapo. Kwa kweli sina matumaini kuwa mambo yatakuwa mazuri. Nimekimbia nyumbani kwangu mara tatu na sina matumaini tena. Ni vigumu kwangu kupanga au kuanza kufikiria kuhusu wajukuu zangu,” anasema Anasthasia akiendelea kupukuchua mahindi na moshi ukifuka pembeni ikiashiria angalau kuna dalili za mlo. 

Mgogoro Ituri ni kati ya kabila la walendu na wahema ambapo mara kwa mara Umoja wa Mataifa umelaani na kusema vitendo hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita.