Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yahimiza uokoaji wa haraka wa wakimbizi wa Rohingya waliokwama majini, Andaman. 

Mwanaume akimsaidia mwanamkde kuelekea ufukweni boti iliyobeba wakimbizi wa Rohingya ilipowasiri Teknaf, Cox's Bazar. (Maktaba)
UNICEF/Patrick Brown
Mwanaume akimsaidia mwanamkde kuelekea ufukweni boti iliyobeba wakimbizi wa Rohingya ilipowasiri Teknaf, Cox's Bazar. (Maktaba)

UNHCR yahimiza uokoaji wa haraka wa wakimbizi wa Rohingya waliokwama majini, Andaman. 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limetoa wito wa kutafutwa na kuokolewa haraka kundi la wakimbizi wa Rohingya ambao  wamekwama katika meli kwenye eneo la maji la Andaman kwa zaidi ya wiki moja.  

Indrika Ratwatte, Mkurugenzi wa Ofisi ya Kanda ya UNHCR ya Asia na Pasifiki, amesema leo kwamba idadi kamili na eneo la waathirika bado halijajulikana, na inaripotiwa kuwa watu wengi wanaweza kuwa wamekufa. 

Ratwatte amesema, "kwa sababu ya ukosefu wa habari sahihi juu ya eneo la wakimbizi, tumewajulisha mamlaka husika za kitaifa juu ya ripoti hizi na kuwaomba watoe msaada wa haraka ikiwa meli hiyo itapatikana katika eneo lake la utafutaji na uokoaji. Hatua ya haraka inahitajika kuokoa maisha. Na zuia majanga zaidi. " 

UNHCR imesema kwamba wakimbizi hawa inadaiwa walitoka Cox's Bazar na Tecnaf kusini mwa Bangladesh takriban siku kumi zilizopita, na boti zao zilikuwa zimekwama baharini kwa sababu ya kushindwa kwa injini, kwa zaidi ya wiki moja iliyopita.  

Wakimbizi wanaripoti kwamba chakula na maji vinakosekana kwenye meli kwa siku kadhaa, na abiria wengi ni wagonjwa. 

Eneo la maji la Andaman ni sehemu ya maji ya Bahari ya Hindi. Iko kusini mashariki mwa Ghuba ya Bengal, kusini mwa Myanmar, magharibi mwa Thailand, na mashariki mwa Visiwa vya Andaman na Nicobar nchini India. 

Kuokoa maisha lazima kiwe kipaumbele cha kwanza. 

UNHCR imetoa wito kwa serikali mbalimbali kupeleka shughuli za utafutaji na uokoaji ili kwa haraka kuwaokoa waathirika,  na kusisitiza kuwa, "kuokoa maisha lazima kiwe kipaumbele." 

Ratwater amehimiza kwamba, "nchi zote zinapaswa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kuwaokoa watu walio katika shida baharini kulingana na majukumu ya kimataifa ya sheria ya bahari na mila ndefu ya baharini, bila kujali utaifa wao au hali yao ya kisheria." 

Aidha Ratwater ameeleza kuwa UNHCR iko tayari kusaidia serikali katika eneo hilo katika siku zijazo kutoa msaada wowote wa kibinadamu na hatua za karantini kwa kadri ya makubaliano ya afya ya umma kwa watu wanaoshuka kutoka katika meli.