Mapinduzi ya kijeshi hayana nafasi karne ya sasa - Guterres

Ukumbi wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo wataalamu wa haki za binadamu huchangia hoja kuhusu haki za binadamu
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Ukumbi wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo wataalamu wa haki za binadamu huchangia hoja kuhusu haki za binadamu

Mapinduzi ya kijeshi hayana nafasi karne ya sasa - Guterres

Haki za binadamu

Mkutano wa 46 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa umeanza hii leo huko Geneva, USwisi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametumia fursa hiyo  kusisitiza mshikamano wake na watu wa Myanmar, wiki tatu baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyosababisha maelfu ya watu kuingia mitaani na kuandamana.
 

“Mapinduzi ya kijeshi hayana nafasi tena katika dunia ya sasa,” amesema Katibu Mkuu katika hotuba yake kwa njia ya video kwa wajumbe wa mkutano huo unaofanyika kwa kiasi kikubwa kwa njia ya mtandao kutokana na janga la Corona au COVID-19.

Guterres amesema “leo hii natoa wito kwa jeshi la Myanar kukomesha ukandamizaji wake mara moja.  Liachie huru wafunjgwa. Liache ghasia. Liheshimu haki za binadamu na utashi wa wananchi uliodhihirishwa kupitia sanduku la kura kwenye uchaguzi wa hivi karibuni. Naunga mkono azimio la Baraza la Haki za Binadamu wa watu wa Myanmar katika kusaka demokrasia, amani, haki za binadamu na utawala wa sheria.”
Kauli ya Katibu Mkuu inafuatia kauli yake ya mwishoni mwa wiki ya kulaani matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa jeshi la Myanmar, kitendo ambacho kimesababisha mauaji ya muandamanaji mmoja na wengine wengi walijeruhiwa.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, iliyotolewa leo mjini Bangoko, Thailand imesema muandamanaji huyo aliyeuawa ni mtoto mwenye umri wa miaka 14 ambapo shirika hilo limesma linalaani matumizi yoyote ya nguvu dihdi ya waandamanaji,  ikiwemo matumizi ya risasi za moto. "UNICEF inatoa wito kwa vikosi vya usalama  kujizuia kufanya ghasia na kutumia nguvu na tofauti zozote zipatiwe suluhu kwa njia ya amani na kupatia kipaumbele usalamwa wa watoto na vijana."

Tweet URL

Naye  Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amemulika zaidi athari hasi za COVID-19.

“Nadhani sote tunatambua kuwa matumizi ya nguvu hayatomaliza hili janga la Coorna. Kusweka jela wapinzani halikadhalika. Vizuizi kinyume cha sheria dhidi ya uhuru wa umma katika kujieleza, kukusanyika na matumizi ya mamlaka kimabavu siyo tu kwamba havisaidii bali pia ni kinyume na kanuni,” amesema Bi. Bachelet.

Amesema kinyume chake vitendo hivyo vinakwamisha ushiriki wa umma katika kupitisha maamuzi, jambo ambalo ni la msingi katika utungaji wa sera bora.

Ujumbe mwingine uliotolewa kwa video kwenye mkutano huo ni kutoka kwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Volkan Bozkir, ambaye amesisitiza umuhimu wa kupatia kipaumbele mahitaji ya msingi ya binadamu ikiwemo chanjo dhidi ya COVID-19 kama njia bora zaidi ya kukwamuka kutoka katika janga la Corona.

“Ni muhimu hatua zote dhidi ya COVID-19 zijikite katika haki za binadamu na ziendeleze ulinzi wa raia wakiwemo walio hatarini zaidi ambao wanahitaji kuangaziwa. Hii inajumuisa mgao sawia wa chanjo. Ni muhimu kwa mashirika ya kiraia , sekta binafsi na wadau wote washirikishwe katika mpango mzima na utoaji wa taarifa za tathmini ya operesheni yote,” amesema Bwana Bozkir.

Akipazia sauti wito wa mgao wa chanjo wenye uwiano kupitia hotuba yake hiyo iliyojikita zaidi dhidi ya watu wenye msimamo mkali wa kibaguzi aliosema ni kitisho kinachovuka mpaka na kitendo cha serakali kutumia takwimu za kidijitali kulaghai wananchi, Bwana Guterres amesema “ukweli kwamba ni nchi 10 tu zilizotoa zaidi ya asilima 75 ya chanjo zote za COVID-19 ni jambo jipya kabisa la janga la kimaadili.”

Uwiano katika chanjo unaashiria haki za binadamu lakini uzalendo kwenye chanjo ni kinyume cha haki za binadamu. Chanjo lazima ziwe bidhaa ya ma na ipatikane na iweze kutumiwa na kila mtu.
Katibu Mkuu ametoa wito kwa nchi wanachama kuchukua hatua zaidi kurejesha wito wa haki za binadamu kimatendo zaidi akitaja maeneo mawili ya kuzingatia kuwa ni adha ya ubaguzi wa rangi, ubaguzi na chuki dhidi ya wageni na pili ukosefu wa usawa wa jinsia.  

Amesema mambo hayo mawili ni muhimu kwa kuwa hivi sasa uzingatiaji wake ni muhimu zaidi na changamoto zitokanazo na mambo hayo ni kubwa na zimesambaa. Aidha, mambo hayo yanazidi kuchochewa na mizizi ya ukosefu wa usawa: ukoloni na mfumo dume hivyo akisema sasa ni wakati wa kuanza upya, kuunda upya, kujenga upya na kuibuka bora zaidi kwa kuzingatia haki za binadamu na utu wa kibinadamu kwa wote. 

Mkutano huo chini ya uongozi wa Balozi Nazhat Shameem Khan wa Jordan, utamalizika Ijumaa tarehe 23 mwezi ujao wa Machi.