Balozi wa Italia DRC auawa katika shambulio Goma: Guterres, WFP walaani

22 Februari 2021

Shirika la Umoja wa Mataaifa la mpango wa chakula duniani WFP, limeelezea kusikitishwa kwake na kutuma salamu za rambirambi kwa familia, wafanyakazi na marafiki wa watu watatu waliouawa leo katika shambulio dhidi ya ujumbe wa ubalozi wa Italia uliokuwa ukizuru mashinani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 

Kwa mujibu wa WFP abiria wengine waliokuwa wakisafiri na ujumbe huo wamejeruhiwa wakati wa shambulio hilo.

 Watu watatu waliopoteza maisha wametambuliwa kuwa ni pamoja na balozi wa Italia nchini DRC Luca Attanasio, afisa wa ubalozi wa Italia na dereva wa WFP. 

Ujumbe huo ulikuwa unasafiri kutoka Goma kuzuru programu ya WFP ya mlo shuleni katika eneo la Rutshuru wakati shambulio hilo lilipotokea. 

WFP imesema itashirikiana na mamlaka ya DRC kubaini taarifa zaidi za waliohusika na shambulio hilo lililotokea katika barabara ambayo iliruhusiwa watu kusafiri bila kusindikizwa na vikosi vya  usalama. 

Hivi sasa WFP inawasiliana na mamlaka ya italia kupitia ofisi zake zilizopo makao makuu ya shirika hilo mjini Roma na pia katika ofisi yao DRC. 

Guterres alaani shambulio ataka wahusika wafikishwe mbele ya sheria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la leo dhidi ya msafara wa pamoja wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP na ubalozi wa Italia huko Kibumba karibu na Goma mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Shambulio hilo lililofanywa na watu wasiojulikana limesababisha vito ya watu watatu akiwemo Balozi wa Italia nchini DRC Luca Attanasio, afisa wa ubalozi wa Italia na dereva wa WFP.

“Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali ya Italia na DRC huku akielezea mshikamano wake na wafanyakazi wa WFP na timu nzima ya Umoja wa Mataifa nchini humo,” imesema taarifa ya msemaji wa Guterres iliyotolewa leo jiijni New  York, Marekani.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa serikali ya DRC kuchunguza haraka tukio hilo na washukiwa wafikishwe mbele ya sheria huku akisema kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia serikali na watu wake katika kusaka amani ya kudumu mashariki mwa nchi hiyo.

 

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter