Tanzania poleni kwa msiba  na chondechonde chukueni tahadhari na toeni takwimu za COVID-19: WHO

20 Februari 2021

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus leo ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Tanzania kwa msiba wa Katibu Mkuu kiongozi wa serikali uliotokea mapema juma hili. 

Kupitia taarifa yake iliyotolewa Jumamosi Dkt. Tedros amesema mwishoni mwa mwezi wa Januari mwaka huu aliungana na Dkt. Matshidiso Moet, ambaye ni mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika kuitaka serikali ya Tanzania kuongeza hatua za kulinda afya ya umma dhidi ya janga la corona au COVID-19 na kujiandaa kwa ajili ya chanjo. 

Pia aliichgiza nchi hiyo ya Afrika Mashariki kutoa takwimu kufuatia ripoti za wagonjwa wa COVID-19 miongoni mwa wasafiri. 

Hata hivyo mkuu huyo wa WHO amesema “Tangu wakati huo nimezungumza na mamlaka kadhaa Tanzania lakini hadi sasa WHO haijapokea taarifa yoyote kuhusu hatua gani Tanzania inachukua kukabiliana na janga hilo la COVID-19.” 

Ameongeza kuwa hali nchini humo inaendelea kutia wasiwasi mkubwa. “Ninarejea wito wangu kwa Tanzania kuanza kutoa taarifa za wagonjwa wa COVID-19 na kutoa takwimu. Pia ninatoa wito kwa Tanzania kutekeleza hatua za afya ya umma ambazo tunafahamu zinaweza kuvunja mnyororo wa maambukizi na kujiandaa kwa chanjo.” 

Dkt. Tedros amesema baadhi ya Watanzania wanaosafiri kwenda nchi za jirani na kwingineko wamepimwa na kubainika kuwa na virusi vya COVID-19. 

“Hii inadhihirisha haja kwa Tanzania kuchukua hatua madhubuti za kulinda watu wake na nchi hizo jirani na kwingineko.” Amesisitiza Dkt. Tedross na kuongeza kuwa COVID-19 ni ugonjwa hatari ambao unaweza kusababisa kuugua hoi na hata kifo. 

Kwa mantiki hiyo amezitaka “Mamlaka za kitaifa kila mahali kufanya kila ziwezalo kulinda watu na kuokoa maisha na kwamba WHO iko tayari kuzisaidia katika hatua za kupambana na virusi hivyo hatari. "

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter