Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2021 tujikwamue, G20 ongozeni mpango wa chanjo duniani- Guterres

Wahudumu wa afya baada ya kupokea chanjo dhidi ya COVID-19 katika hospitali nchini India.
UNICEF/Vinay Panjwani
Wahudumu wa afya baada ya kupokea chanjo dhidi ya COVID-19 katika hospitali nchini India.

Mwaka 2021 tujikwamue, G20 ongozeni mpango wa chanjo duniani- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amehutubia mkutano wa Munich wa masuala ya usalama hususan vipaumbele vya hatua za kimataifa ambapo ametaja mambo makuu manne ya kuzingatia ili kuwezesha dunia kujikwamua salama kutoka athari za majanga yanayokumba dunia likiwemo lile la ugonjwa wa Corona au COVID-19 pamoja na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatishia amani na usalama na duniani.

Amesema changamoto za Corona, zikigubikwa na ukosefu wa uthabiti katika kushughulikia janga hilo hasa utoaji chanjo kwa uwiano, changamoto za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usawa pamoja na rushwa vinazidi kuweka hali tete duniani.

Ni kwa mantiki hiyo akataja vipaumbele vyake ili mwaka 2021 uwe mwaka wa kusonga kwa pamoja ambapo mosi ni mpango wa kimataifa wa utoaji chanjo akisema, “chanjo lazima zipatikane kwa kila mt una kila mahali. Uwiano katika usambazaji na upataji wa chanjo ni muhimu katika kuokoa maisha na kunusuru uchumi. Nchi lazima ziendelee kupatiana chanjo za ziada na zitoe mabilioni ya fedha zinazohitajiwa na mfumo wa kimataifa wa kusaka na kusambaza chanjo, COVAX.”

G20 iunde kikosi kazi cha dharura kuhusu mpango wa chanjo

Amerejelea wito wake kuwa ana imani kundi la nchi 20 au G20 zina uwezo wa kuanzisha kikosi kazi cha dharura na kuandaa mpango huo wa pamoja na kuleta pamoja nchi, kampuni na taasisi za kimataifa zenye uwezo wa kifedha na utaalam wa kisayansi na uzalishaji wa chanjo.

Kipaumbele cha pili ni kuondokana kabisa na uzalishaji wa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050.

Kipaumbele cha tatu ni “kuondokana na mivutano baina ya pande mbalimbali duniani na badala yake kuimarisha diplomasia ya amani. Hatuwezi kutatua matatizo yetu makubwa ilhali mataifa yenye nguvu yanavutana. Dunia yetu haiwezi kuwa na mustakabali bora ambamo kwamo nchi mbili zenye uchumi mkubwa duniani zinavutana na kugawanya dunia katika pande mbili za mvutano.”

Ametumia mkutano huo kukumbushia wito wake wa sitisho la mapigano duniani akisema inatia matumaini kuwa katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa na mizozo sugu, hali imetulia lakini kwingineko bado mapigano yanaendelea.

Sitisho la mapigano

Lakini zaidi ya yote sitisho hilo la mapigano lisiishie kwenye viwanja vya mapigano tu bali pia majumbani, sehemu za kazi, shuleni na kwenye usafiri wa umma ambako wanawake na wasichana wanakabiliwa na janga la ghasia.

Mapigano ya kikabilia yameathiri jamii Pibor mashariki mwa Sudan Kusini.
UN Photo/Isaac Billy
Mapigano ya kikabilia yameathiri jamii Pibor mashariki mwa Sudan Kusini.

Kipaumbele cha nne ni kupanga upya utawala na usimamizi wa karne hii ya 21 akisema, “kanuni zetu za msingi lazima ziweze kuhimili karne ya 21. Hii ina maana kuhakikisha mbinu mpya za kusambaza huduma kwa umma, kujenga utandawazi ulio sawia na kutatua changamoto za pamoja.  Hatuhitaji urasimu mpya. Lakini tunahitaji kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ambao tayari upo duniani. Kupitia mashirika ya kikanda.”

Katibu Mkuu amesema huu ni wakati wa mshikamano na ushirikiano wa kimataifa kushughulikia changamoto kubwa zaidi na ngumu, “ninashawishika kuwa iwapo tumeazimia, tunaweza kufanikisha malengo yetu ya pamoja.”