Tubadili mtazamo la sivyo safari ya kutokomeza ubaguzi wa rangi bado ndefu- Guterres

18 Februari 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema safari ya kutokomeza ubaguzi wa rangi na madhila yatokanayo na kitendo hicho bado ni ndefu sana kwa kuzingatia kile kinachoshuhudia hivi sasa ulimwenguni kote.

Bwana Guterres amesema hayo wakati akihutubia mkutano maalum wa mawaziri wa Baraza la kiuchumi na kijamii la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ECOSOC jijini New York Marekani hii leo, mkutano ambao maudhui yake ni kutazama upya usawa kwa kutokomeza ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na ubaguzi wote katika muongo huu wa Umoja wa Mataifa wa kufanikisha ajenda 2030 au malengo ya maendeleo endeleu, SDGs.

"Ubaguzi wa rangi umepoozesha dunia yetu. Unachukiza, ni mbaya na uko kila pahali. Lazima tuulaani bila kizuizi chochote na bila kusita. Ubaguzi ni kukataa utu wetu wa pamoja uliomo ndani ya Chata ya Umoja wa MAtaifa," amesema Bwana Guterres.

Katibu Mkuu amesema ubaguzi wa rangi na ukosefu wa usawa kwa misingi ya rangi vimeota miziz ikwenye taasisi, mifumo ya kijamii na katika maisha ya kila siku.

Amehoji kulikoni? Na akajibu kuwa "kwa kiasi kikubwa ubaguzi wa rangi umeoteshwa mizizi na karne za ukoloni na utumwa. Ukosefu wa haki kwa misingi ya rangi, hususan kwa watu wenye asili ya Afrika, umesababisha kiwewe na machungu ya kizazi hadi kizazi."

Waandamanaji Brooklyn, New York Marekani wakiandamana kwa amani kuhusu ukosefu wa haki na ubaguzi wa rangi
UN News/ Shirin Yaseen
Waandamanaji Brooklyn, New York Marekani wakiandamana kwa amani kuhusu ukosefu wa haki na ubaguzi wa rangi

Nyufa za ubaguzi zimeonekana dhahiri wakati wa COVID-19

Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limefichua ukosefu huo wa usawa na kudhihirisha mfumo ulioota mizizi wa upendeleo na ubaguzi. "Katika baadhi ya maeneo, viwango vya vifo ni vikubwa mara tatu zaidi kwa watu wa pembezoni au kipato cha chini. Ukosefu wa huduma unaenda sambamba na rangi ya mtu au kabila lake. Na athari za janga hili linapasua zaidi misingi ya ubaguzi kama vile jinsia, umri, daraja, dini, ulemavu, mrengo wa jinsia pamoja na hadhi ya kiuchumi, kijamii na kisheria."

Tuchukue hatua zaidi ya kulaani pekee

Katibu Mkuu anaona jawabu ni kuchukua hatua badala ya kusalia kutoa matamko ya kulaani kwa kuwa kutokomeza ubaguzi si shughuli ya mara moja wakati huu ambapo Katibu Mkuu anasema dunia inashuhudia "kuyoyoma kwa maadili ya ustaarabu au ufahamu ambayo ni stahmala, kuheshimiana. Badala yake tunashuhudia ongezeko la uzawa, umaarufu usio na maslahi ya umma, chuki dhidi ya wageni, hata watu kuona ubora zaidi kwa watu weupe na unazi mamboleo."

Kundi la watu wakikataana na chuki na ubaguzi unaotegemea kabila na dini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. (2017)
OCHA/Yaye Nabo Sène
Kundi la watu wakikataana na chuki na ubaguzi unaotegemea kabila na dini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. (2017)

Ubaguzi ni adui wa kufanikisha ajenda 2030

Guterres amsema ubaguzi unaweka mkwamo kwa watu kupata fursa kama elimu, ajira, huduma za afya na haki wale waliokuwa wameachwa nyuma, wanazidi kusalia nyuma.

"Tunapohaha kujikwamua kutoka katika janga na kujenga dunia bora zaidi, tunahitaji mkataba mpya wa kijamii kwa misingi ya ujumuishi na uendelevu. Hii ina maana kuwekeza katika mtangamano wa kijamii," amesema Katibu Mkuu.

Amesisitiza kuwa kadri jamii zinavyozidi kuwa na watu tofauti kwa misingi ya makabila, rangi, dini na tamaduni, "tunahitaji uwekezaji mkubwa wa kisiasa, kitamaduni, kiuchumi ambao ni jumuishi ili kuweza kuvuna faida za utoaji huo badala ya kuuona kama tishio."

Kila kundi lazima liweze kuona tofauti zao zinaheshimiwa huku likijihisi kuwa ni sehemu inayoheshimika katika jamii nzima.

Hata hivyo amesema hilo linamaanisha uwazi, huduma zipatikane kwa usawa na kwa wote na ushiriki wa watu wote wakiwemo wale wa pembezoni au makundi madogo.

Katibu Mkuu amesema kupitia ajenda 2030 au malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, "tunaweza kufanikisha usawa na haki kwa watu wote na kutokomeza aina zote za ubaguzi."

Amesema yeye yuko tayari kushiriki katika kusongesha mbele ajenda hiyo.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter