Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa ILO Comoro wapatia wenyeji ajira zenye staha 

Watu wanaoishi katika visiwa vya Comoro kwenye bahari ya Indi wanahitajhi kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
UNDP Comoros/James Stapley
Watu wanaoishi katika visiwa vya Comoro kwenye bahari ya Indi wanahitajhi kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Mradi wa ILO Comoro wapatia wenyeji ajira zenye staha 

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Comoro, shirika la kazi duniani, ILO limetekeleza mradi wa kuinua maisha ya wakazi wa vijijini unaotoa fursa kwa wananchi kushiriki katika ajira zenye staha za ujenzi wa barabara na hivyo kufungua milango zaidi ya mauzo ya mazao yao ya kilimo na hatimaye kuondoa umaskini.

Mkoani Mboinkou katika kisiwa kikuu cha Comoro barani Afrika, wananchi wake kwa waume wakiwa katika ujenzi wa barabara, mradi wa kazi kwa ujira na maendeleo, EDLIC unaotekelezwa na ILO

Wananchi hawa walipatiwa mafunzo ya ujenzi wa barabara zao ili kufungua maeneo mapya ya kilimo na hivyo kuongeza siyo tu mavuno bali pia kipato chao katika jamii hii ambayo wakazi wengi ni wakulima lakini umaskini umeghubika. 

Dola Elfu 40 zilitolewa kupitia chama cha ushirika kwa mafunzo ya wakulima 100 kwenye mkoa wa Mboinkou  na walipatiwa pia vifaa vya kisasa vya kilimo yakiwemo majembe 5 ya kisasa. 

Moullida Msaidie ni kutoka chama cha ushirika cha Ri Ridhi na anasema, “unaweza kuona kazi iliyokamilishwa na ushirika wa Ri Ridhi kwa faida yetu. Barabara hii itaturahisishia mambo yetu na kutuletea faida nyingi.” 

Kwa upande mwingine wanaushirika wa kikundi kingine cha Raouni wanaonekana wakiwa shambani wakisaka mawe ya kujenga barabara zao. 

Katibu Mkuu wa kikundi hicho Bahia Ally anasema, “kwa sababu ya janga la COVID-19 hakuna hata mmoja wetu anayeweza kwenda kufanya kazi. Kwa hiyo wengi wetu tunajikuta mashambani. Na sasa tuna soko Shezani tunapata machenza, nyanya na kadha wa kadha. Na hii ni vema kutokana na vikwazo vya kutembea mijini.” 

Akizungumzia mradi huu na faida zake, Meya wa mji wa Mboinkou, Nakib Ali Soilihi amesema,“Katika muktadha wa maendeleo ya kilimo katika eneo la Mboinkou, tunashukuru ILO kwa mradi huu wa nguvu kazi ya vibarua kwa sababu una faida; mosi mavuno yamekuwa bora, pili ni ajira katika jamii. Tunatarajia kuendelea kufanya kazi na ILO ili kuimarisha kilimo kwa mkoa huu na nchi kwa ujumla,”