Skip to main content

Walimu kote duniani wanafanya kazi kwa ajili ya matokeo na si kipato-Mwalimu bora duniani 

Mwalimu Ranjitsinh Disale mshindi wa Tuzo ya kimataifa ya Mwalimu bora duniani kwa mwaka 2020.
Vaibhav Gadekar
Mwalimu Ranjitsinh Disale mshindi wa Tuzo ya kimataifa ya Mwalimu bora duniani kwa mwaka 2020.

Walimu kote duniani wanafanya kazi kwa ajili ya matokeo na si kipato-Mwalimu bora duniani 

Utamaduni na Elimu

Mwalimu Ranjitsinh Disale kutoka katika jimbo la Maharashtra ambaye ndiye mshindi wa mwaka wa Tuzo ya kimataifa ya Mwalimu bora duniani kwa mwaka 2020, amesema tuzo ya dola milioni 1 aliyoipata atagawana na washindani wenzake 9 waliofika ngazi ya fainali ili wakaendeleze elimu katika maeneo yao. 

Mwalimu Ranjitsinh Disale, baada ya mchujo wa zaidi ya  washiriki 12,000 kutoka nchi 140 ndiye aliibuka mshindi kutokana na ubunifu wake ambao umetokomeza ndoa za utotoni, kuongeza mahudhurio na ufaulu hususani kwa wasichana katika shule ya msingi ya Zilla Parishad katika Kijiji cha Paritewad, Maharashtra India. Alianza kwa kuwavutia watoto kuja shule kwa kuwaonesha video katika kompyuta yake, kisha akapata wazo la kuwafikia walioko mbali zaidi na shule.  

Katika mahojiano na Anshu Sharma wa Idhaa ya kihindi ya Umoja wa Mataifa, Mwalimu Disale anasema, «Siku moja nilipoenda dukani, nikamwona muuzaji anatumia mashine ya kusoma namba za bidhaa yaani QR Code, kisha bei inaonekana kwenye kopyuta, wakati huo huo kitu kikanijia kichwani. Ninaweza kufanya hii. Nikarudi nyumbani nikaanza kurambaza katika mitandao na kuona ninachoweza kufanya na kinachoweza kuwekwa. » 

Baada ya hapo Mwalimu huyu alianza kutumia utaalamu huo kuweka vitabu na masomo katika vifaa vya kielektroniki ambapo wanafunzi wanaweza kujisomea na kujadiliana wakiwa maeneo tofauti. Pia aliunda mfumo ambao unawakumbusha wazazi kila jioni saa moja, kuwasaidia watoto wao, kazi za shule.  

Kuhusu tuzo yake ya dola milioni moja, anasema anagawana nusu na wengine tisa walioshindana naye kwani, «Walimu kote duniani wanafanya kazi kwa ajili ya matokeo sio kipato. Walimu mara zote wanashirikiana kwa mtazamo, ujuzi, maarifa, taarifa na wanafunzi. Kwa nini tusigawane fedha yetu ya tuzo pia. Kugawana kwangu fedha, lengo langu ni kuunga mkono kazi nzuri ambayo wanaifanya darasani. Fedha hii itawahamasisha kuendelea namna ambavyo wamekuwa wakifanya. » 

Tuzo ya mwalimu bora wa mwaka duniani, ni tuzo ya heshima ambayo hutolewa kila mwaka kwa ushirikiano na shrika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO kwa mwalimu ambaye ameleta mabadiliko chanya si tu katika shule yake bali katika jamii inayomzunguka kwa ujumla. 

Mchakato wa maombi na uteuzi wa Tuzo ya mwalimu bora duniani ya mwaka huu 2021 umefunguliwa tarehe pili ya mwezi huu wa Februari na utafungwa mnamo tarehe 30 Aprili mwaka huu. 

Mwaka 2019 tuzo hii ilishindwa na mwalimu Peter Tabichi kutoka Kenya  kufuatia kujitolea kwake kwa hali na mali katika kufanikisha utendaji wa wanafunzi wake katika shule ya sekondari ya Keriko iliyoko kaunti ya Nakuru nchini Kenya.