Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP: Sudan Kusini iko katika hatihati ya baa kubwa la njaa

Watoto wakila uji uliopikwa na mama yao baada ya kupokea mgao kutoka kwa WFP, Pibor nchini Sudan Kusini.
WFP/Marwa Awad
Watoto wakila uji uliopikwa na mama yao baada ya kupokea mgao kutoka kwa WFP, Pibor nchini Sudan Kusini.

WFP: Sudan Kusini iko katika hatihati ya baa kubwa la njaa

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP linasema Sudan Kusini ipo katika hatihati ya baa kubwa la njaa kwani inakabiliwa na viwango vya hali ya juu ya kutokuwa na uhakika wa chakula kuwahi kushuhudiwa tangu taifa hilo changa zaidi duniani kupata uhuru wake yapata miaka 10 iliyopita.

Katika kijiji cha kaunti ya Vertet jimboni Jonglei mizoga ya mifugo mitaani inadhihirisha athari za mafuriko makubwa yaliyokumba eneo hili ambalo pia WFP inasema, katika nusu ya kwanza ya 2020 pamoja na kaunti zingine sita ambazo ni vigumu kuzifikia machafuko yalitawala na hivyo kuwafanya maelfu ya watu kufungasha virago na kukimbia. 

Baadhi ya watu hao wamepoteza maisha, na wengine wengi kila kitu ikiwemo vyanzo vya chakula.  

Wakulima hawakuweza tena kulima na wengine wameibiwa mifugo yao au imekufa kutokana na magonjwa na mafuriko.

Sasa wako katika hatari kubwa ya baa la njaa, miongoni mwao ni mjane wa watoto wanne Nyal Chol Liech ,“Nilikuwa katika taharuki mafuriko yalipokuja, hakuna aliyenisaidia, mume wangu aliuawa vitani, kila mtu katika eneo letu alikimbia na nikabaki peke yangu na wanangu, lakini nilichagua kubaki. Hofu ya mimi na wananagu kutokuwa na malazi na kuishia kuombaomba chakula ilikuwa kubwa zaidi ya hofu ya mafuriko.” 

WFP inasema asilimia 60 ya watu wote wa Sudan Kusini sawa na watu milioni 7.24 wanakabiliwa na njaa, na hali hiyo inawaweka watoto pabaya zaidi hasa kupata utapiamlo. Kavagochi Koli ni mjane mwingine mwenye watoto watano,“Wakati chakula kinapokwisha na chungu kusalia kitupu hapo ndipo maisha yanapoanza kuwa msumari wa moto juu ya kidonda kwetu"

Hivi sasa WFP imeongeza msaada wa dharura kwa kaunti hizo sita zilizoathirika vibaya na mwaka huu inatarajia kuwafikia watu zaidi ya milioni 5.3 kwa msaada wa chakula na lishe lakini pia programu nyingine za kuwawezesha mamilioni hayo ya watu kuishi.