Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 222 kunusuru zasakwa kusaidia wakimbizi wa Burundi Tanzania, Rwanda na DRC

Mtoto mkimbizi kutoka Burundi akikamilisha kaiz yake ubaoni kwenye shule ya msingi ya Jugudi huko kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma nchini Tanzania. (Februari 2019)
© UNHCR/Farha Bhoyroo
Mtoto mkimbizi kutoka Burundi akikamilisha kaiz yake ubaoni kwenye shule ya msingi ya Jugudi huko kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma nchini Tanzania. (Februari 2019)

Dola milioni 222 kunusuru zasakwa kusaidia wakimbizi wa Burundi Tanzania, Rwanda na DRC

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, na wadau wake 33 wametoa ombi la dola milioni 222.6 kuwezesha kusambaza misaada muhimu ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Burundi kwa mwaka huu wa 2021.
 

Taarifa ya  UNHCR iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi imesema fedha hizo ni kwa ajili ya wakimbizi wa Burundi ambao kwa takribani miaka saba sasa wanaishi ukimbizini huko Rwanda, Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
“Ingawa mpito wa kisiasa nchini Burundi mwaka jana ulileta matumaini kwa wakimbizi wengi kuwa wanaweza kurejea nyumbani, bado idadi kubwa ya warundi wataendelea kuhitaji ulinzi wa kimataifa mwaka wote wa 2021,”  imesema taarifa hiyo.

Fedha hizo zinalenga kuwapatia wakimbizi hao msaada muhimu kama vile chakula, elimu, malazi pamoja na huduma za afya na maji safi, huduma ambazo ni muhimu katika kuhakikisha mikakati ya ulinzi hasa wakati huu wa janga la Corona.

Akizungumzia ombi hilo, Mkurugenzi wa UNHCR kanda ya Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu, Clementine Nkweta-Salami amesema suala la jamii ya kimataifa kuongeza msaada ni muhimu ili kuhakikisha wakimbzi hao wa Burundi wanapata huduma bora na wanazostahili wanapokuwepo nchi jirani.

Pamoja na huduma hizo muhimu , fedha hizo zitaelekezwa pia katika mipango ya kuwezesha wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiari na kiutu, mpango wa pamoja unaojumuisha mapokezi, ufuatialiaji na kuwawezesha wakimbizi kujumuika tena kwenye jamii zao Burundi.

Ombi la mwaka huu linakuja wakati ombi la mwaka 2020 la dola milioni 293 kusaidia wakimbizi wa Burundi lilikuwa miongoni mwa maombi ambayo hayakuchangiwa vya kutosha kwa kupata asilimia 40 pekee.

Matokeo yake maisha ya wakimbizi wa Burundi yalikuwa si ya kuridhisha hata mgao wa chakula ulipunguzwa, malazi si bora sambamba na huduma zisizotosheleza za dawa na shughuli za kujipatia kipato.