Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TANZBATT_7 yafunga virago DRC na kukabidhi kijiti kwa TANZBATT_8

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu MONUSCO nchini DRC wakizungumza na wananchi wakazi wa jimbo la Kivu Kaskazini.
TANZBATT_8/Kapteni Tumaini Bagambo.
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu MONUSCO nchini DRC wakizungumza na wananchi wakazi wa jimbo la Kivu Kaskazini.

TANZBATT_7 yafunga virago DRC na kukabidhi kijiti kwa TANZBATT_8

Amani na Usalama

Kikosi cha 7 cha Tanzania, TANZBATT_7 kwenye kikosi maalum cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO kimetamatisha jukumu lake rasmi na kukabidhi bendera kwa kikosi cha 8 au TANZBATT_8. Shuhuda wetu kutoka Beni, jimboni Kivu Kaskazini ni Luteni Issa Mwakalambo, afisa habari wa TANZBATT_7. 

Luteni Kanali John Magnus Ndunguru, Kamanda wa kikosi TANZBATT_7 cha MONUSCO ambacho kiliwasili Beni jimboni Kivu Kaskazini mwezi Oktoba mwaka 2019 na anasema “tulifika maeneo ya Beni, hali ya usalama haikuwa nzuri sana na raia hawakuwa na uwezo wa kufanya shughuli zao kutokana na vikundi vya waasi. Lakini kwa juhudi zetu kwa kuzingatia mamlaka na maelekezo ya Umoja wa Mataifa, kwa kushirikiana na jeshi la serikali ya DRC, FARDC, tumefaulu kufanikisha kwa kiasi fulani, walau raia katika maeneo wanayotuzunguka wanaweza kufanya shughuli zao vizuri na wanaendelea na majukumu yao vizuri.” 

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
Kikosi kimoja chaaga kingine chapokea mikoba DRC!

Kwa upande wake Kamanda wa kikosi TANZBATT_8 Luteni Kanali Fortunatus Nassoro anasema, “kikubwa ni kwamba mimi sitaanza upya, bali nitaendeleza pale wenzangu walipoachia. Kama alivyosema mwenzangu, amani ya DRC, hasa eneo tumekalia, imeimarika kwa kiasi kikubwa. Ni mambo madogo madogo tu ndiyo yanaendelea na ambayo yako ndani ya  uwezo wetu. Wenzetu wametekeleza wajibu wao kuwafikisha pale walipowafikisha na hata sisi siyo peke yetu, tuko vikundi vingi tunashirikiana pamoja. Vikundi vya Malawi, Afrika Kusini na  jeshi la serikali, tuna mshikamano mkubwa sana katika utendaji na eneo la uwajibikaji.” 

Katika hatua nyingine, Luteni Kanali Ndunguru kupitia idara ya TEHAMA ya TANZBATT_7 ametoa vyeti vya kuhitimu mafunzo ya kompyuta kwa raia vijana wa DRC ikiwa ni mchango wa kusaidia raia kupata elimu hiyo kupitia wataalamu wa kikundi hicho kinachotamatisha jukumu la ulinzi wa amani jimboni Kivu Kaskazini.