Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya nguvu dhidi ya raia Myanmar hayakubaliki- Guterres

Jua likizama kwenye mji wa Yangon nchini Myanmar.
Unsplash/Alexander Schimmeck
Jua likizama kwenye mji wa Yangon nchini Myanmar.

Matumizi ya nguvu dhidi ya raia Myanmar hayakubaliki- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya hali inayoendelea nchini Myanmar, ikiwemo ongezeko la matumizi ya nguvu kupita kiasi na kuongezwa kwa vifaru vye kijeshi kwenye miji mikuu nchini humo.
 

Taarifa ya msemaji wake iliyotolewa jijini New York, Marekani siku ya Jumapili immemnukuu Bwana Guterres akitoa wito kwa polisi na jeshi nchini Myanmar wahakikishe wanaheshimu haki ya watu kukusanyika na waandamanaji hawakumbwi na visasi.

“Ripoti za kuendelea kwa ghasia, vitisho na manyanyaso kutoka vikosi vya usalama hazikubaliki,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa matukio ya kuendelea kukamatwa kwa viongozi wa kisiasa, maafisa wa serikali, wanachama wa mashirika ya kiraia na wawakilishi wa vyombo vya habari yanatia wasiwasi mkubwa, sambamba na vizuizi vya mtandao wa intaneti na huduma za mawasiliano.

Bwana Guterres amesema huduma hizo hazipaswi kuzuiwa ili kuhakikisha haki ya uhuru wa kujieleza, ambao unajumuisha pia haki ya mtu kupata taarifa.

Katibu Mkuu amesisitiza wit wake kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa pamoja na kwa uhusiano wao na Myanmar, kuangalia jinsi ya kushawishi suala la ulinzi wa haki za binadamu na haki za msingi kwa watu wa Myanmar.

Amesisitiza usaidizi thabiti wa Ukmoja wa Mataifa kwa watu wa Myanmar katika harakati zao za kusaka demokrasia, amani, haki za binadamu na utawala wa kisheria.

Halikadhalika ametoa wito kwa mamlaka za kijeshi kumruhusu haraka mjumbe wake maalum kwa Myanmar, Christine Schraner Burgener ili aweze kutembelea taifa hilo la barani Asia kwa masharti yanayokubalika ili aweze kujionea mwenyewe hali halisi.

Hali ya sintofahamu imekuwa ikikumba Myanmar tangu mapinduzi ya kijeshi ya Januari 31 mwaka huu yaliyoondoa madarakani serikali ya kiraia iliyokuwa ikiongozwa na Rais Win Myint na  kiongozi mkuu Aung San Suu Kyi.