Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Historia yaandikwa: Ngozi Okonjo-Iweala Mkurugenzi Mkuu WTO

Dkt. Ngozi Okonjo-Iweala wa Nigeria, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirka la Biashara Duniani, WTO.
© WTO/Jay Louvion
Dkt. Ngozi Okonjo-Iweala wa Nigeria, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirka la Biashara Duniani, WTO.

Historia yaandikwa: Ngozi Okonjo-Iweala Mkurugenzi Mkuu WTO

Masuala ya UM

Ngozi Okonjo-Iweala kutoka Nigeria amechaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika la biashara duniani, WTO.
 

Taarifa iliyotolewa leo na WTO imesema “wanachama wa WTO leo wamefanya historia pale walipokubaliana kwa kauli moja kumchagua Ngozi Okonjo-Iweala wa Nigeria kuwa Mkurugenzi Mkuu wa saba wa chombo hicho.”
Anaanza jukumu lake tarehe 1 mwezi Machi mwaka huu na anakuwa mwanamke wa kwanza na mwafrika wa kwanza kuchaguliwa kushika wadhifa huo na awamu ya kwanza itamalizika tarehe 31 mwezi Agosti mwaka 2025.

“Huu ni wakati wa kipekee kwa WTO. Kwa niaba ya Baraza Kuu, natuma salamu zangu za pongezi kwa Dkt. Ngozi Okonjo-Iweala kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO na ninamkaribisha katika mkutano huu wa Baraza Kuu,” amesema Mwenyekiti wa Baraza hilo David Walker kutoka New Zealand ambaye yeye na waratibu wenza Balozi Dacio Castillo (Honduras) na Balozi Harald Aspelund (Iceland) waliongoza mchakato wa uchaguzi wa Mkurugenzi Mkuu wa WTO, mchakato ambao umefanyika kwa miezi tisa.

Amemshukuru Dkt. Ngozi kwa uvumilivu wake wakati wa miezi hiyo tis ana kwamba ana matumaini kuwa wanachama wa shirika hilo watashirikiana naye vyema katika kipindi cha uongozi wake ili kusongesha mbele harakati za WTO.

Dkt. Ngozi azungumza

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo, Dkt. Okonjo-Iweala amesema kipaumbele chake kikuu ni kushirikiana na wanachama kushughulikia haraka athari za kiuchumi na kiafya zilizoletwa na janga la Corona au COVID-19.

“Ni heshima kubwa kuchaguliwa na wanachama kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WTO. WTO thabiti ni muhimu sana katika kujikwamua haraka na vyema kutoka katika mvurugano uliosababishwa na janga la COVID-19. Natarajia kushirikiana na wanachama kutekeleza sera za kuchukua hatua ili turejeshe tena uchumi wa dunia mahali pake.”

Mchakato wa uchaguzi

Uamuzi wa leo wa Baraza Kuu la WTO unafuatia hali ya sintofahamu iliyoibuka baada ya Marekani awali kukataa kuunga mkono maridhiano ya kumchagua Dkt. Okonjo-Iweala na badala yake kuonesha kumuunga mkono Waziri wa Biashara wa Korea Kusini Yoo Myung-hee.

Hata hivyo kufuatia uamuzi wa Bi. Yoo wa tarehe 5 mwezi huu wa Februari wa kujiondoa kwenye mchakato, utawala mpya wa Marekani chini ya Rais Joe Biden ulitupilia mbali kizuizi cha Marekani na kutangaza kumuunga mkono kwa dhati Dkt. Okonjo-Iweala.

Balozi Walker ameshukuru wagombea wote wanane walioshiriki kwenye mchakato huo, hususan Bi. Yoo “kwa kuendelea kuunga mkono WTO na mifumo yake ya biashara ya kimataifa.”

Mchakato wa kumchagua Mkurugenzi Mkuu mpya wa WTO ulianza tarehe 14 mwezi Mei mwaka 2020 baada ya Mkurugenzi Mkuu Roberto Azevêdo kujulisha nchi wanachama wa shirika hilo kuwa anan’gatuka kutoka wadhifa huo, mwaka mmoja kabla ya kumaliza kipindi chake. Aliondoka rasmi tarehe 31 mwezi Agosti mwaka jana.