Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto huko Tigray wanahitaji ulinzi na msaada- UNICEF

UNICEF imesambaza huduma za kujisafi na usafi kwa wakimbizi wa ndani huko Shire jimboni Tigray nchini Ethiopia.
© UNICEF/Esiyei Leul Kinfu
UNICEF imesambaza huduma za kujisafi na usafi kwa wakimbizi wa ndani huko Shire jimboni Tigray nchini Ethiopia.

Watoto huko Tigray wanahitaji ulinzi na msaada- UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Kadri misaada ya dharura na wafanyakazi wa kusambaza misaada hiyo wanafikia eneo la mzozo la Tigray huko Ethiopia, taswira halisi ya masikitiko inazidi kuibuka jinsi watoto kwenye eneo wanavyoendelea kuteseka.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema , idadi kubwa ya familia zimetenganishwa wakati wa kukimbia mapigano na miongoni mwa wakimbizi wa ndani ni watoto ambao wamekimbia wenyewe bila mzazi au mlezi.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo Addis Ababa Ethiopia, Nairobi Kenya, Geneva Uswisi na New York Marekani imesema kuwa kati ya tarehe 4 na 7 mwezi huu wa Februari, timu ya shirika hilo ilifika mji wa Shire katikati ya Tigray Kati ikiwa na malori 6 yaliyosheheni misaada ya dharura, ikiwa ni shehena ya kwanza tangu mapigano yaanze Tigray tarehe 4 mwezi Novemba mwaka jana.

“Mji huo ni makazi ya watu 170,000 lakini sasa una takribani wakimbizi wa ndani 52,000 na wengine wengi wameendelea kuwasili. Hakuna maji ya kunywa kwa kuwa mtambo wa maji mjini humo haufanyi kazi, kwa hiyo UNICEF na chama cha kimataifa cha hilal nyekundu, ICRC wanasafirisha maji kwa gari hadi kwa wakazi na wakimbizi. Wakimbizi wengi wa ndani wanaishi kwenye shule, ambazo hakuna hata moja inafanya kazi. Mazingira ya makazi ya wakimbizi hao wa ndani yanasikitisha, vyoo vichache vilivyopo vimeharibika, hakuna maeneo ya kuogea na maji safi na salama ni kidogo mno,” imesema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa UNICEF, familia nyingi zimeripoti kuwa na msongo wa kisaikolojia na zina hofu kurejea nyumbani kutokana na wasiwasi kuwa hata siku za usoni wanaweza kukumbwa na mashambulio kule walikokimbia.

Hospitali mjini Shire

Hali ya vituo vya afya mjini Shire nayo si nzuri ambapo UNICEF inseam hospitali moja inafanya kazi kwa kiwango kidogo vituo viwili kati ya vinne vilikuwa vinatoa huduma kwa wagonjwa wanaokuja kupata huduma na kurejea nyumbani, sambamba na kwa wajawazito. WAfanyakazi nao hawajapata malipo yao ya ujira kamilifu huku vituo vya afya nje ya mji huo navyo haviko vizuri kwa kuwa baadhi yao vimeporwa vifaa vyao.

Mahitaij yetu ni chakula

Wakimbizi wa ndani wanasema hivi sasa wanahitaji chakula wakati huu ambapo tathmini ya haraka imebaini kuwa kuna tatizo la utapiamlo uliokithiri ambao ni wa kutisha hasa ukichanganyika na magonjwa kama vile kipindupindu au surua, kiwango ambacho ni asilimia 2.1. UNICEF inasema kiwango hicho ni juu ya kile cha shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO.
Hofu ni uwezekano wa kulipuka magonjwa kwa kuzingatia ukosefu wa maji salama, huduma za kujisafi na usafi sambamba na huduma za afya.

Hadi mwisho wa mwezi Januari, UNICEF kwa ushirikiano na serikali ya Ethiopia na wadau huko Tigray na maeneo jirani imeshachukua hatua kadhaa za dharura ikiwemo kupima zaidi ya watoto 450,000 wenye  umri wa chini ya miaka 5 kama wana utapiamlo na kuwapatia huduma za kuokoa maisha kwa wale waliobainika kuwa na utapiamlo.

Halikadhalka imefikishi watu 137,000 wakiwemo wakimbizi wa ndani na wenyeji huduma za maji safi na salama. Halikadhalika wasichana barubaru na wanawake 5,400 wamepatiwa vifaa vya kujisafi.