Alama ya ng’ombe ni ujasiri na uthabiti na tutumie kujikwamua 2021- Guterres

12 Februari 2021

Chun Jie Kuai Le! Ndivyo alivyoanza ujumbe wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika kuadhimisha kuanza kwa mwaka mpya wa kachina, akimaanisha Heri ya Mwaka Mpya wa Kichina!

Katibu Mkuu amesema anatuma salamu zake za heri kwa kila mtu anayeadhimisha mwaka huu mpya ambao alama yake mwaka huu ni ng’ombe.

“Mwaka huu ni mwaka wa ng’ombe ambao ni alama sawa na mwaka wangu wa kuzaliwa. Ng’ombe anaashiria nguvu uthabiti na ujasiri,” amesema Guterres

Amesema sifa hizo za ng’ombe ni sifa ambazo dunia inahitaji hivi sasa katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 ambalo hadi sasa limesababisha vifo vya watu milioni 2.3 kati ya wagonjwa zaidi ya milioni 106 duniani kote.

Janga la COVID-19

Mwaka jana janga la COVID-19 limeleta ukosefu mkubwa wa uhakika na mvurugano, amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa mwaka huu wa 2021 “ni lazima tusimame pamoja kukabili virusi, tuchukue hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na tujenge hatua bora za kukwamuka kutoka katika janga.”

Katibu Mkuu ameishukuru China na wananchi wake kwa kuendelea kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa na Umoja wa Mataifa katika mihimili yote ya kazi ya chombo hicho chenye wanachama 193.

“Natarajia kuendelea kwa ushirikiano wetu. Natuma salamu zangu za heri kwa ajili ya ustawi, afya na furaha kwa mwaka huu wa ng’ombe,” ametamatisha ujumbe wake Katibu Mkuu huku akishukuru akisema Xie Xie kwa kichina akimaanisha, Asante!

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter