Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mnyumbuliko mpya wa virusi vya COVID-19 ni changamoto kwa watengenezaji wa chanjo- COVAX 

Chanjo ya COVID-19.
Novavax/Elliott O'Donovan
Chanjo ya COVID-19.

Mnyumbuliko mpya wa virusi vya COVID-19 ni changamoto kwa watengenezaji wa chanjo- COVAX 

Afya

Mpango wa kimataifa wa kuratibu chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19, COVAX, umesema kuibuka kwa minyumbuliko tofauti ya virusi aina ya SARS-CoV-2 vinavyosababisha COVID-19 ni kumbusho thabiti kuwa virusi hivyo vina uwezo wa kubadilika na hivyo hatua za kisayansi zinapaswa kuendana na mazingira ili ziweze kukabili virusi hivyo. 

Mashirika yanayounda mpango wa COVAX yamesema hayo katika taarifa ya pamoja iliyotolewa katika miji ya Geneva,  Uswisi, Oslo Norway na New York, Marekani kufuatia ripoti za hivi majuzi ya kwamba chanjo dhidi ya Corona aina ya AstraZeneca/Oxford ina uwezo mdogo wa kuzuia ugonjwa Corona usababishwao na mnyumbuliko mpya wa virusi B.1.351

Taarifa hiyo imesema kuwa ni muhimu kutambua kuwa uchambuzi wa msingi kutoka awamu ya tatu ya majaribio ya chanjo hiyo hadi sasa bila kuwepo kwa mnyumbuliko huo mpya wa virusi, ina uwezo wa kinga dhidi ya ugonjwa wa Corona unapokuwa katika hali mbaya zaidi, kama vile mgonjwa akiwa hospitalini au anakaribia kifo. 

Kwa mantiki hiyo COVAX inasema ni muhimu sana hivi sasa kubaini uthabiti wa chanjo pindi linapokuja suala la kinga pindi mgonjwa anapokuwa taabani baada ya kuambukizwa aina mpya ya virusi vya Corona. 

Taarifa hiyo imesema uchambuzi zaidi utawezesha pia kuthibitisha ratiba sahihi ya utoaji wa chanjo hiyo na ufanisi wake. 

Kwa upande wake watengenezaji wametakiwa kujiandaa juu ya mabadiliko ya virusi aina ya SARS-CoV-2 ikiwemo kutoa chanjo za kuongeza nguvu na ziendanazo na virusi vilivyopo iwapo itaonekana lazima kufanya hivyo, 

Mapema akizungumzia minyumbuliko ya virusi,  Dkt. Richard Hatchett, ambaye ni Afisa Mtendaji wa Ushirika wa ubunifu wa maandalizi dhidi ya milipuko ya magonjwa, CEPI, amesema,  “Unafahamu tulitarajia bila shaka virusi hivyo vinaweza kubadilika. Wanasayansi kwenye maabara walitarajia hivyo na hii ndio moja ya mambo mazuri kwenye sayansi. Inakuwezesha kuangazia siku za usoni na mambo yanayoweza kutokea na kuangazia mabadiliko yanayoweza kuleta madhara.” 

Hata hivyo COVAX imeendelea kusisitiza kuchukuliwa kwa kila hatua kupunguza kusambaa kwa virusi, kuzuia maambukizi yanayoweza kutoa fursa zaidi ya virusi SARS-CoV-2 kunyumbulika na kupunguza ufanisi wa chanjo za sasa.