Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikunde ni suluhu ya njaa na kulinda mazingira:FAO 

Mikunde na matunda yaliyokaushwa kwenye soko la Esquilino Roma, Italia.
Photo FAO/Marco Salustro
Mikunde na matunda yaliyokaushwa kwenye soko la Esquilino Roma, Italia.

Mikunde ni suluhu ya njaa na kulinda mazingira:FAO 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya mikunde duniani, shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO linasema kuna kila sababu ya kuipenda mikunde sio tu kwa kuwa suluhu ya njaa bali pia uwezo wake wa kulinda na kuhifadhi mazingira.

Kwa mujibu wa FAO mikunde ni muhimu katika kushughulikia changamoto za umasikini, uhakika wa chakula, afya ya binadamu na lishe, afya ya udongo na mazingira, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika malengo ya maendeleo endelevu ,SDGs na pia kwa mradi wa FAO ujulikanao kama mkono kwa mkono 

Maudhui ya siku ya mwaka huu ni “Penda mikunde kwa ajili ya afya na sayari” FAO inasema siku hii ni muhimu kwa ajili ya kuelimisha umma juu ya faida za lishe za mikunde na mchango wake katika mifumo endelevu ya chakula na kuwa na dunia bila njaa. 

Shirika hilo limeongeza kuwa faida za mikunde ni lukuki tukianza na afya ya binadamu “ni chanzo cha gharama nafuu cha protini, pia mikunde imesheheni vitamini mbalimbali, haina chumvi nyingi, haina mafuta, inadumu kwa muda mrefu na ina madini mengine ambayo yanaweza kusaidia kuzuia magonjwa kama kisukari na matatizo ya moyo.” 

Na kwa upande wa sayari mikunde imeelezwa kuwa “ni mizuri kwa afya ya udongo kwani inazalisha hewa ya nitrojeni ambayo inarutubisha ardhi, pia aina nyingi za mikunde huvumilia ukame, hazihitaji maji mengi, na zina mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.” 

Hata hivyo FAO inasema pamoja na faida zote hizo, mikunde imepoteza umaarufu wake katika miaka ya karibuni na matumizi yake duniani kote yamepungua kwa sababu ya ongezeko la kipato miongoni mwa walaji na pia walajai kupendelea vyakula vingine zaidi ya mikunde. 

Kwa mantiki hiyo katika siku hii ambayo huadhiumishwa kila mwaka Februari 10 FAO inasisitiza umuhimu wa kuelimisha umma kuhusu faida za mikunde kwa binadamu, sayari, mazingira na ufikiaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs.