'Kuna uwezekano mkubwa' kuwa virusi vya COVID-19 havikuanzia kwenye maabara Wuhan- Wataalamu

9 Februari 2021

Jopo la wataalamu wa kimataifa wanaochunguza chanzo cha virusi vya ugonjwa wa Corona, au COVID-19 kwenye jimbo la Wuhan nchini China, wametupilia mbali nadharia ya kwamba virusi hivyo vilitoka katika maabara, huku wakisema utafiti zaidi unahitajika.

Mkuu wa ujumbe wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, kwenye msafara huo, Peter Ben Embarek amewaambia waandishi wa habari hii leo mjini Wuhan nchini China kuwa “hakuna uwezekano kwamba virusi hivyo vilivuja kutoka maabara kwenye mji wa Wuhan.”

Hata hivyo amesema kazi zaidi inapaswa kufanyika ili kubaini chanzo cha virusi hivyo ambavyo hadi sasa vimesababisha watu milioni zaidi ya 106 duniani kote kuugua na kati yao milioni 2.3 wamefariki dunia.

Kwa mujibu wa Dkt. Embarek, “uchunguzi wao umebaini taarifa mpya lakini haujabadilisha kwa kiasi kikubwa taswira ya mlipuko wa COVID-19. Matokeo yetu ya awali yanadokeza kuwa virusi hivyo viliingia kwa binadamu kupitia kiumbe kingine na hiyo itahitaji uchunguzi zaidi na utafiti lengwa zaidi.”

Wakazi wa Wuhan wakinunua bidhaa katika soko moja kwenye eneo hilo nchini China mwezi Aprili mwaka jana baada ya shughuli kufunguliwa tena kufuatia zuio la siku 76 kutokana na Corona.
Wang Zheng
Wakazi wa Wuhan wakinunua bidhaa katika soko moja kwenye eneo hilo nchini China mwezi Aprili mwaka jana baada ya shughuli kufunguliwa tena kufuatia zuio la siku 76 kutokana na Corona.

Popo hawako Wuhan!

Wakati tafiti zinazoendelea zinadokeza kuwa popo wanaweza kuwa wabebaji wa virusi vya Corona, Dkt. Embarek amesema hakuna uwezekano huo kwa sababu mji wa Wuhan hauko karibu na mazingira ambako popo wanapatikana.
Nadharia moja inadokeza kuwa virusi hivyo vinaweza kuwa vimetokea katika mnyonyoro wa vyakula vilivyogandishwa kwa barafu na kisha kuambukiza binadamu.

Dkt. Embarek amesema bidhaa za nyama zilizogandishwa kwenye barafu, hususan vya baharini vilikuwa vinauzwa kwenye soko la Huanan, sambamba na nyama za wanyamapori na wa kufugwa  na baadhi walitoka maeneo mengine ya China au waliagizwa kutoka nje ya nchi,

“Kwa hiyo kuna uwezekano wa kuendelea kufuatilia mwenendo huo na kuangalia zaidi mnyonyoro wa usambazaji wa bidhaa na wanyama ambao walifikishwa sokoni wakiwa wamegandishwa kwenye barafu au wengine waliokuwa wamesindikwa au wabichi,” amesema Dkt. Embarek.

Janga la COVID-19

Akizungumza kwenye mkutano huo, Dkt. Lian Wannian, ambaye aliongoza jopo la China kwenye ujumbe huo amesema uchunguzi uliofanywa na jopo hilo Wuhan unaweka msingi wa kufuatilia chanzo cha virusi hivyo kwingineko.

Amesema tathmini yao kwenye tafiti ambazo bado hazijachapishwa unadokeza kuwa virusi hivyo vilikuwepo tayari vinasambaa katika maeneo mengine kabla hata ya kugunduliwa Wuhan.

Dkt. Wannian amesema baadhi ya sampuli shukiwa zilibainika mapema sana kabla hata ya kuripotiwa mgonjwa wa kwanza na hiyo inadokeza uwezekano ya kwamba baadhi ya visa havikuripotiwa katika maeneo mengine.

Halikadhalika amesema utafiti wao umegundua kuwa hakuna dalili yoyote ya kwamba kulikuwepo na maambukizi ya COVID-19 mjini Wuhan kabla ya Desemba 2019.

Jopo husika

Jopo hilo la kimataifa liliundwa na WHO likihusisha wataalamu 17 kutoka China na wengine 17 kutoka mataifa mengine wakiangalia kuenea kwa ugonjwa, utafiti wa kimolekyuli, wanyama na mazingira.

Wakati wa ziara yao walitembelea hospitali na maeneo mengine jijini Wuhan likiwemo soko la Huanan ambako mgonjwa wa kwanza wa virusi vya Corona aina ya SARS-CoV-2 alibainika na waliibuka na nadharia kuu nne ya jinsi virusi hivyo vinaweza kuwa vilisambazwa kwa binadamu.

Tayari mwaka mmoja umepita tangu COVID-19 itangazwe kuwa dharura ya afya ya umma duniani.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter