Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Mkuu wa UNHCR aisihi jumuiya ya kimataifa kuiunga mkono Colombia kuwasaidia wavenezuela

Wakimbizi kutoka Venezuela wanaokimbia njaa wanavuka mpaka Cúcuta, Colombia na kutembea hadi miji mingine.
WFP/Jonathan Dumont
Wakimbizi kutoka Venezuela wanaokimbia njaa wanavuka mpaka Cúcuta, Colombia na kutembea hadi miji mingine.

Kamishna Mkuu wa UNHCR aisihi jumuiya ya kimataifa kuiunga mkono Colombia kuwasaidia wavenezuela

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi akiwa ziarani Colombia amesema ukarimu wa Colombia katika kukaribisha wakimbizi wa Venezuela haupaswi kuchukuliwa kwa urahisi na akaomba msaada wa kimataifa kuunga mkono juhudi za nchi hiyo ambazo zinaendelea kulinda watu waliokimbia makazi yao licha ya changamoto za janga la COVID-19. 

Katika eneo la Paraguachón ambao ni mpaka kati ya Colombia na Venezuela, wakimbizi kutoka Venezuela wanaendelea kuvuka kuingia Colombia.  

Wakimbizi na wahamiaji wanaokadiriwa kuwa milioni 5.4 hivi sasa wanaishi nje ya Venezuela kwa kuwa wamekimbia uhaba mkubwa wa chakula na dawa na ukosefu wa usalama nchini mwao  na hali hiyo kuufanya kuwa mgogoro wa makazi wa pili kwa ukubwa duniani baada ya ule wa Syria.  

Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi ameitembelea Colombia ambayo inaendelea kuwapokea wakimbizi ingawa nayo iko katika kupambana na madhara ya janga la virusi vya corona na anasisitiza umuhimu wa kuwatambua na kuwarasimisha wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela ilI kuhakikisha ujumuishwaji wao katika jamii na wakati huo huo akisifia juhudi za serikali ya Colombia katika kulishughulikia hilo….Anasema, “Tumekutana na familia na watu, na hadithi zao mbaya za safari hatari. Shida kuu hapa Colombia ni kwamba kwa watu wengi wa Venezuela, wanabaki katika hali ya kukosa hadhi yoyote, na ukosefu huu wa kuwarasimisha unawatenga, unawaadhibu. Serikali inafanya kazi kwa bidii kujaribu kupata suluhisho la shida hii, kwa sababu kuwatambua kutamaanisha kwamba wavenezuela wanaokuja Colombia wanaweza kupata ajira, kufanya kazi na wanaweza kupata huduma, afya, elimu, kwa namna inayoweza kutabirika . ” 

Bwana Grand pia amekutana na wakimbizi kama Veronica, ambaye analea watoto wanne peke yake, mmoja Franyimar mwenye umri wa miaka mitano ambaye ana ulemavu unaomfanya ashindwe kutembea vizuri. Familia hii ilivuka kuingia Colombia kupitia mpaka usio rasmi ili kutafuta matibabu ya mtoto huyu. Walitumia takribani wiki moja wakilala mitaani hadi pale walipokipata kituo cha usaidizi kinachofadhiliwa na UNHCR kwa kushirikiana na serikali ya Colombia. Verónica Petit anasema,  "Kuwa na kitambulisho halali nchini Colombia kutafanya watu waseme ‘Tazama, ana kitu kinachomruhusu kufanya kazi na kulea watoto wake na kuwapa elimu.' Inamaanisha ulimwengu kwangu kuwa katika nchi hii. " 

Sasa katika Kituo hicho, Veronica amepokea dawa ya kutibu hali ya binti yake. Veronica na watoto wake pia wamepokea msaada wa kisaikolojia na kisheria na kurasmisha hali zao nchini Colombia.  

Colombia ni mwenyeji wa wavenezuela milioni 1.7na zaidi ya nusu ya wakazi wa Venezuela wa Colombia wanakosa hadhi ya kawaida ya uraia, na hivyo kuathiri uwezo wao wa kupata huduma muhimu, ulinzi na usaidizi.