Skip to main content

Ninachotaka ni eneo ambalo halifuriki- Manusura wa Eloise 

Kimbunga Eloise kimepiga Msumbiji Praia Nova, Beira.
UNICEF Mozambique/Ricardo Franco
Kimbunga Eloise kimepiga Msumbiji Praia Nova, Beira.

Ninachotaka ni eneo ambalo halifuriki- Manusura wa Eloise 

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Msumbiji, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limechukua hatua kusaidia manusura wa kimbunga Eloise kilichopiga eneo la Beira jimboni Sofala mwishoni mwa mwezi uliopita ambapo sasa manusura waliokumbwa na mafuriko wanajengewa makazi ya muda sambamba na kuwekewa huduma za kujisafi na maji safi.

Ujenzi wa makazi ya muda! Uchimbaji wa vyoo vya shimo! Huduma za majisafi na salama! 

Ni eneo la Beira, wakimbizi wa ndani waliofurushwa na kimbunga Eloise wakiwa wamesaka hifadhi eneo hili, wakiwa na nyuso za matumaini kutokana na UNICEF kuanza kuwafikishia huduma za msingi, mbali na kwao walikozoea. 

 Miongoni mwao ni Ana Bonabe, mwenye umri wa miaka 39 na anakumbuka hali ilivyokusa akisema, “Tumekuja hapa kwa sababu ya mafuriko. Ilikuwa Jumatatu na ilipotokea. Tulikuwa tumejificha kwenye shule ya Mungasa walipokuja na basi kutuchukua. Shule yote ilisambaratishwa. Nyumba yote iliporomoka, hadi sasa kuna maji mengi. Walipotutoa shuleni walituleta hapa. Kimbunga kilipopiga tulishafika hapa.” 

 Akizungumzia anachotaka hivi sasa anasema, “kile ninachotaka sasa ni mahali pamdogo ambako hakufuriki ili nisitaabike tena na mafuriko. Nimepoteza nyumba,  nguo, shajara ya mtoto, vyote vimelowana. Na nyaraka pia! Hakuna jinsi yoyote ya kuvipata tena kwa kuwa vimeharibika.” 

Tayari UNICEF imefika hapa na Daniel Timme, mkuu wa mawasiliano UNICEF yuko makini kuona kazi ya kufunga mahema inafanyika vyema sambamba na uchimbaji wa vyoo akisema,“Tunajenga vyoo haraka na ni muhimu kwa sababu tunataka kuepusha magonjwa yatokanayo na maji machafu kama vile Kipindupindu na tunafanya hivi kwa ajili ya watu 2,000 kutoka kijiji cha Rema ambao wamesaka hifadhi hapa Beira, kando mwa shule ya Samora Machel, sasa wanaishi kambini.” 

 Virago vya familia ndani ya hema, sambamba na mtoto akiwa amelala huku mtoto mwingine akifua nguo na tabasamu licha ya machungu wapitiayo huku wanawake wakiendelea na mapishi. Katika kisima cha maji safi, huduma inaonekana kuwa mkombozi ambapo familia zinateka maji na angalau kuna matumaini ya mlo na kuepuka magonjwa kwa sasa.