Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola DRC: UNICEF yachukua hatua kudhibiti kuenea 

Karatasi ya plastiki imetenganisha mama na mwanae atika kituo cha matibabu ya ebola Beni, Kivu Kasakzini nchini DRC.
© UNICEF/Thomas Nybo
Karatasi ya plastiki imetenganisha mama na mwanae atika kituo cha matibabu ya ebola Beni, Kivu Kasakzini nchini DRC.

Ebola DRC: UNICEF yachukua hatua kudhibiti kuenea 

Afya

Kufuatia serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kutangaza kifo cha mtu mmoja huko Butembo jimboni Kivu Kaskazini kutokana na ugonjwa wa Ebola, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limepeleka wafanyakazi zaidi na linajiandaa kupeleka vifaa vya matibabu. 

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini imesema pamoja na hatua hizo, inasaidiana na mamlaka kufuatilia wale wote waliokuwa karibu na marehemu huyo ambaye ni mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka 42. 

Tayari wafanyakazi wa UNICEF kutoka ofisi ya Beni, wamefika Butembo kusaidia na kitengo cha afya mjini humo wakati huu ambapo shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, nalo pia limeshachukua hatua za kupeleka wataalamu na kubaini watu waliokuwa karibu na marehemu. 

UNICEF pia imesema inaongeza wafanyakazi wengine wa masuala ya mawasiliano ili kusaidia kuhamasisha jamii kwenye maeneo alimopatikana mgonjwa huyo ili kuhakikisha hatua sahihi zinachukuliwa kufuatialia waambata na pia kufahamisha wale ambao wanapaswa kupatiwa chanjo dhidi ya Ebola

Vifaa vya matibabu vitasafirishwa kutoka Mbandaka jimboni Equateur. 

Kwa mujibu wa mamlaka za DRC, marehemu ambaye alikuwa mke wa manusura wa Ebola, alikwenda kituo cha afya cha Biena kilichoko kilometa 90 kusini-magharibi mwa Butembo tarehe Mosi mwezi huu wa Februari akiwa na dalili zinazofanana na ugonjwa wa Ebola. 

Alifanyiwa uchunguzi na hatimaye kuhamishiwa hospitali ya Matanda mjini Butembo ambako alifariki dunia tarehe 3 mwezi Februari na uchunguzi ulithibisha kuwa alikuwa na Ebola. 

Majimbo ya Kivu Kaskazini, Ituri na Kivu Kusini yalikumbwa na mlipuko wa Ebola, wa pili kwa ukubwa duniani mwezi Agosti mwaka 2018. 

Mlipuko huo ulidumu kwa miezi 23 na kuua watu 2,287 kati ya 3470 waliougua ugonjwa huo, asilimia 28 wakiwa ni watoto. 

Wakati wa mlipuko huo, UNICEF ilipatia vituo 3,812 vya afya huduma za msingi kama vile maji safi na salama, huduma za kujisafi sambamba na kuwapatia watoto 16,000 msaada wa kisaikolojia huku zaidi ya watu milioni 37 nchini DRC wakipatiwa taarifa muhimu ili kujikinga na Ebola.