Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola yaibuka tena DRC, mgonjwa afariki dunia

Katika eneo la Butembo mashariki mwa DR Congo, wafanyakazi wa shirika la Msalaba Mwekundu wakiwa katika mavazi maalumu ili  kukinga kusambaza ugonjwa wa Ebola wakati wa maziko. (Agosti 2019)
UN Photo/Martine Perret
Katika eneo la Butembo mashariki mwa DR Congo, wafanyakazi wa shirika la Msalaba Mwekundu wakiwa katika mavazi maalumu ili kukinga kusambaza ugonjwa wa Ebola wakati wa maziko. (Agosti 2019)

Ebola yaibuka tena DRC, mgonjwa afariki dunia

Afya

Wizara ya afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, imetangaza kupatikana kwa mgonjwa mpya wa Ebola kwenye mji wa Butembo jimboni Kivu Kaskazini, eneo ambalo lilikuwa kitovu cha mlipuko wa 10 uliotangazwa kumalizika mwezi Juni mwaka jana.

Taarifa ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, kanda ya Afrika iliyotolewa leo huko Brazaville Congo imesema mgonjwa huyo amefariki dunia na alikuwa mke wa manusura wa Ebola.

Taasisi ya utafiti wa magonjwa, nchini DRC, INRB tawi la Butembo lilithibitisha sampuli kutoka kwa mgonjwa huyo aliyekuwa amelazwa kwenye kituo cha afya mjini humo kuwa ni Ebola.

Kutokana na uwezo wa enoo hili kudhibiti mlipuko wa awali wa Ebola, hivi sasa mamlaka za Afya jimboni Kivu Kaskazini kwa msaada wa WHO zinaongoza harakati za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

WHO ilikuwa imepatia mamlaka hizo mafunzo kwa wataalamu wa maabara, wafuatiliaji wa waambata wa wagonjwa wa Ebola, wataalamu wa utoaji chanjo sambamba na miradi ya kusaidia manusura wa Ebola.

Akizungumzia taarifa za uwepo wa Ebola Kivu Kaskazini, Mkurugenzi WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti, amesema “WHO inasaidia mamlaka za afya za kitaifa nae neo la Kivu Kaskazini kufuatilia haraka, kutambua na kutibu waambata wa marehemu ili kudhibiti kuenea zaidi kwa virusi vya Ebola.”

Hivi sasa wataalamu wa tiba wa WHO wako Kivu Kaskazini kuchunguza kisa hicho. Hadi sasa zaidi ya watu 70 wametambuliwa kuwa walikuwa na makaribiano na mgonjwa huyo aliyefariki dunia na kazi ya kutakasa maeneo aliyokuwa ametembelea inaendelea.

Sampuli zake pia zimepelekwa katika maabara kuu ya INRB kwenye mji mkuu Kinshasa, ili kutambua mnyumbuliko sahihi wa virusi hivyo vya Ebola na hatimaye kuona kama ni vile vile vya mlipuko wa awali au ni tofauti.

Mlipuko wa 10 wa Ebola nchini DRC ulidumu kwa takribani miaka miwili na ulikuwa ni mlipuko wa pili kwa ukubwa duniani ukiwa na wagonjwa 3481 ambapo kati yao hao 2299 walifariki dunia na 1162 walipona.

Harakati za kukabili mlipuko huo zilikuwa zinakumbwa na changamoto kutokana na ukosefu wa usalama kwenye eneo hilo.