Kamanda wa zamani wa LRA akutwa na hatia na ICC pasipo shaka yoyote

4 Februari 2021

Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC, imempata na hatia za jumla ya makosa 61 Dominic Ongwen, kamanda wa zamani wa kundi la Lord’s Resistance Army, LRA la Uganda. 

Makosa hayo yanajumuisha uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa Kaskazini mwa Uganda kati ya tarehe 1 Julai 2002 na 31 Desemba 2005. 

Akizungumza mjini Hague Uholanzi hii leo Februari 04, Jaji Kiongozi Bertram Schmitt amesema, "Dominic Ongwen amepatikana na hatia pasina shaka yoyote ya uhalifu kadhaa uliofanywa katika muktadha wa mashambulizi manne yaliyotajwa kwenye kambi za wakimbizi wa ndani za Pajule, Odek, Lukodi na Abok - mashambulio dhidi ya raia, mauaji, jaribio la mauaji, mateso, utumwa, kudhalilisha utu binafsi, uporaji, uharibifu wa mali na mateso. 

Majaji wa ICC walipotembelea kaskazini mwa Uganda mnamo mwezi Juni 2018 kama sehemu ya ufuatiliaji wa kesi dhidi ya kamanda wa zamani wa LRA, Dominic Ongwen.
© ICC-CPI
Majaji wa ICC walipotembelea kaskazini mwa Uganda mnamo mwezi Juni 2018 kama sehemu ya ufuatiliaji wa kesi dhidi ya kamanda wa zamani wa LRA, Dominic Ongwen.

 

Ongwen pia amehukumiwa kwa makosa kadhaa ya kingono na ya kijinsia aliyoyafanya dhidi ya wanawake saba waliotekwa nyara na kuwekwa ndani ya nyumba yake, pamoja na ndoa ya kulazimishwa, kuteswa, kubakwa, utumwa wa kijinsia, utumwa, mimba ya kulazimishwa na udhalilishaji. 

Kamanda huyo wa zamani wa LRA pia amepatikana na hatia kwa uhalifu kadhaa wa kingono na wa kijinsia aliowatendea wasichana na wanawake ndani ya brigedi ya Sinia, uhalifu ambao ni ndoa ya kulazimishwa, mateso, ubakaji, utumwa wa kijinsia na utumwa. Pia amehukumiwa kwa uhalifu wa kuwaingiza watoto walio chini ya umri wa miaka 15 katika kikosi cha Sinia na kuwatumia kushiriki kikamilifu katika ukatili. 

 

Mahakama imegundua kuwa uhalifu huu ulifanywa katika muktadha wa uasi wenye silaha wa Jeshi la Lord Resistance (LRA) dhidi ya serikali ya Uganda. LRA, pamoja na Dominic Ongwen, waliwatambua raia wanaoishi Kaskazini mwa Uganda kama wanaohusishwa na serikali ya Uganda, na hivyo kama adui. Hii ilihusu hasa wale ambao waliishi katika kambi zilizoanzishwa na serikali za wakimbizi wa ndani. 

Jopo la mahakama liligundua kuwa Dominic Ongwen anahusika kikamilifu na uhalifu huu wote, “mahakama haikupata ushahidi uliounga mkono madai kwamba alikuwa na ugonjwa wowote wa akili au shida wakati wa kipindi kinachohusiana na mashtaka au kwamba alifanya uhalifu huu kwa kulazimishwa au kwa vitisho vyovyote.” Imesema ICC.  

Kufuatia uamuzi huu, Mahakama itatoa adhabu kwa Dominic Ongwen, baada ya kupokea maoni juu ya hukumu inayofaa kutoka kwa Mwendesha Mashitaka, timu ya utetezi ya Ongwen, na wawakilishi wa kisheria wa waliotahirika ambao wanashiriki katika kesi hii.   

Mkataba wa kuanzisha ICC, Mkataba wa Roma, hautoi adhabu ya kifo; adhabu inaweza kuwa hadi miaka 30 ya kifungo, na katika mazingira ya kipekee kifungo cha maisha. Zaidi, awamu nyingine kwa ajili ya  fidia kwa waathirika itafunguliwa. 

Uamuzi huu unaweza kukatiwa rufaa na upande wowote unaohusika na kesi hii ndani siku 30 baada ya taarifa ya hukumu. 

Dominic Ongwen alikuwa kamanda wa brigedi wa kikosi cha Sinia cha Lord's Resistance Army. Alishtakiwa kwa makosa 70 ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita. 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter