Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaadhimisha siku ya udugu duniani, Guterres apokea tuzo

Msichana kutoka Kenya akisomea nyumbani wakati wa vikwazo kukabiliana na janga la COVID-19.
© UNICEF/Brian Otieno
Msichana kutoka Kenya akisomea nyumbani wakati wa vikwazo kukabiliana na janga la COVID-19.

UN yaadhimisha siku ya udugu duniani, Guterres apokea tuzo

Utamaduni na Elimu

Leo ni siku ya udugu duniani ambayo imeadhimishwa kwa mara ya kwanza ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema dunia hivi sasa inahitaji udugu kuliko wakati wowote ule.
 

Katika ujumbe wake hii leo, Bwana Guterres amepongeza nchi wanachama kwa kuridhia uwepo wa siku hii kupitia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, akizitaja zaidi Falme za Kiarabu na Misri ambazo zilikuwa mstari wa mbele kusongesha mchakato wake.

Katibu Mkuu amegusia pia umuhimu wa azimio la mwaka 2019 la Udugu wa kibinadamu kwa ajili ya amani duniani na kuishi kwa pamoja.

Azimio hilo lilipitishwa kwa pamoja na kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis na Imam Mkuu wa Al-Azhar Sheik Ahmed Al-Tayeb, ambapo Guterres amesema azimio hilo ni muundo wa imani ya pamoja na mshikamano wa binadamu.

Katibu Mkuu ameshukuru viongozi hao wa kidini kwa kutumia sauti zao kuendeleza mazungumzo baina ya imani mbalimbali za kidini, kuheshimiana na maelewano baina ya dini mbalimbali.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, zama za sasa zinahitaji fikra na misimamo ya aina hiyo kuliko wakati wowote ule.
Katibu Mkuu amesema duniani kote, ubaguzi umeota mizizi, ukosefu wa stahmala na uhalifu utokanao na vitendo vya chuki dhidi ya watu kwa misingi yao ya kidini au imani zao, kabila au jinsia zao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kushoto) alipokutana na Papa Francis mjini Vatican Roma 20 Desemba 2019
UN Photo/Rein Skullerud
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kushoto) alipokutana na Papa Francis mjini Vatican Roma 20 Desemba 2019

Kwa Katibu Mkuu, “vitendo vya aina hiyo ni kinyume na makubaliano ya haki za binadamu za kimataifa na maadili ya Umoja wa Mataifa. Tofauti za kitamaduni na imani mbalimbali za uhuru ni sehemu ya utajiri wa ustaarabu wetu.”

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu wa Umoja amesema katika maadhimisho haya ya kwanza ya siku ya udugu duniani, “hebu tusongeshe utamaduni, stahamala ya kidini, maelewano na mashauriano baina yetu.”

Tukio

Maadhimisho haya ya leo yameandaliwa kwa pamoja na jumuika la ustaarabu la Umoja wa Mataifa, UNAOC na ubalozi wa Misri na Falme za Kiarabu kwenye Umoja wa Mataifa, tukio lililofanyika kwa njia ya mtandano.

Katibu Mkuu na tuzo ya udugu

Siku hii pia imeshuhudia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Guterres akipotea tuzo ya Zayed ya udugu wa kibinadamu aliyopatiwa kwa kutambua mchango wake katika kusongesha amani na utu wa kibinadamu kila siku na kila pahali kupitia Umoja wa Mataifa.

Amempongeza pia Latifa Ibn Ziaten wa Ufaransa ambaye wamepokea pamoja tuzo hiyo, ambapo Latifa amepatiwa tuzo hiyo kwa jitihada zake za kusaidia vijana hasa wenye asili ya kiarabu kuepuka kulazimishwa kuingia kwenye misimamo mikali.

Tuzo hii ilianzishwa mwaka 2019 kwa kutambua michango ya watu au mashirika katika kuweka fursa za maendeleo ya kibinadamu na awali imeshapatiwa Papa Francis na Imam Mkuu wa Al Azhar Dkt. Ahman al Tayeb.

Katibu Mkuu amesema tuzo hiyo itakuwa ni ushawishi mkubwa wa kuendeleza kaiz muhimu na ameamua dola 500,000 zitokanazo na tuzo hiyo zielekezwe kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR ili kusaidia wale waliofurushwa makwao.